Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri wa kodi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe Emmanuel Luhahula akizungumza wakati wa kikao cha ushauri wa kodi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Mji -Mjini Kiomboi tarehe 29 Disemba 2020. Kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba na mwingine ni Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba Ndg Novline Munuo. (Picha Zote Na Mathias Canal)
Na Mathias Canal, Iramba-Singida
Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri wa kodi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe Emmanuel Luhahula amempongeza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba Ndg Novline Munuo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaimarika.
Dc Luhahula ametoa pongezi hizo tarehe 29 Disemba 2020 wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha ushauri wa kodi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mjini Kiomboi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe ambao ni Meneja TRA Wilaya ya Iramba Ndg Novline Munuo, Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt Mwigulu Nchemba, Katibu Tawala Wilaya ya Iramba Ndg Sango Songoma, Mkuu wa Usalama wa Taifa Wilaya ya Iramba Ndg Nick Chilale, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Iramba Ndg Peter Lusesa, Mwenyekiti wa wafanyabiashara ambaye ni Diwani wa kata ya Kiteka Mhe Wilfred Kizanga, Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Mji wa Kiomboi ambaye ni Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Ndg Romwald Mwendi pamoja na wajumbe wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya.
Mhe Luhahula amesema kuwa wakati Meneja huyo anaanza kazi katika wilaya hiyo kulikuwa na mashine 4 za EFD lakini kwa muda mfupi kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mashine hizo kwani zimefikia 86 ikiwa ni ongezeko la asilimia zaidi ya 96%.
Pamoja na pongezi hizo lakini Mkuu huyo wa Wilaya ya Iramba ameitaka Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba kuongeza juhudi za ukusanyaji kodi kwani miradi mingi inayofanywa na serikali kwa ajili ya huduma mbalimbali inatokana na kodi za wananchi.
Amesema kuwa ongezeko la ulipaji kodi ndio chachu ya ongezeko la shughuli mbalimbali za huduma za maendeleo katika jamii huku akisisitiza kuwa kulipa kodi ni alama ya uzalendo na sio adhabu kwani ni sehemu ya mpango wa kuongeza mapato ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.
“Kulipa kodi ni alama ya uzalendo na sio adhabu ni mpango wa Serikali kuipeleka mbele nchi kimapato na kukua uchumi wake”, Amekaririwa Mhe Luhahula.
Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa kulipa kodi ni mchango wa lazima ambao umewekwa kisheria kwa raia na wageni kwa lengo la kukusanya mapato kwa ajili ya matumizi ya Taifa.
Akizungumzia masuala ya makadirio, Waziri Nchemba aliitaka mamlaka hiyo kuhakikisha wanatenda haki kwa kuangalia uhalisia wa biashara au huduma inayotolewa kwa sababu unaweza kumpa mtu makadirio ya bei ya juu badala ya kumsaidia ukidhani kwamba ndio utapata kodi kumbe umechochea kufungwa biashara.
“Mkiwapa kodi ambayo ni halali watajua ni wajibu wao na wataweza lakini niwaambie kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inawapenda walipa kodi na wafanyabiashara hivyo wahimizwe kuhakikisha wanalipa kodi” Alisema
Amesema kuwa ulipaji wa kodi ndio uti wa mgongo wa Taifa lolote hivyo hawana budi kujipanga vizuri kuhakikisha watumishi wa TRA na wafanyabiashara hawajengeani mazingira ya chuki na walipa kodi ambao ni wananchi.
Wajumbe wa kikao cha ushauri wa kodi Wilaya ya Iramba kwa kauli moja wameridhia umuhimu wa kutolewa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
MWISHO