***************************************
Na Ezekiel Mtonyole – Manyoni.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika kijiji cha Makanda imeezua paa la shule ya Sekondari Makanda iliyopo katika kijiji cha Makanda, Kata ya Makanda Wilayani Manyoni Mkoani Singida.
Akizungumza mara baada ya kufika katika shule hiyo Mbunge wa Manyoni Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Dkt Pius Chaya amesema jana alipigiwa simu na uongozi wa kijiji wakimtaarifu juu ya madhara hayo.
” Jana nilipigiwa simu na kujulishwa juu ya kuezuliwa kwa paa la shule na mimi nikawataarifu viongozi wenzangu na tukaweka mikakati kuhakikisha madarasa haya yanarudishwa katika hali yake” amesema Dkt Chaya.
Amesema yeye kwa kushirikiana na viongozi katika Wilaya hiyo watahakikisha wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha shule zinapofunguliwa madarasa hayo yanakuwa tayari yamekarabatiwa.
“Tayari tumeweka mikakati ndani ya siku saba (7) tuwe tumekamilisha madarasa haya wanakijiji wameahidi kutoa mbao na mimi na wenzangu tutashughulikia suala la bati zinahitajika kama 90 hivi na hili lipo ndani ya uwezo wetu” amesema.
Amesema licha ya tatizo hilo bado wanaupungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati amebainisha kuwa kwa kushirikiana na viongozi wengine watahakikisha wanalifanyia kazi tatizo hilo mapema kabla ya ukomo wa zoezi hilo uliowekwa na Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema anafahamu kuwa hosteli ya shule hiyo imekamilika lakini haina vitanda wala magodoro hivyo yeye kama Mbunge atahakikisha anafanikisha hilo mapema kama alivyoahidi kipindi cha kampeni, sambamba na ujenzi wa Ofisi ya walimu katika shule hiyo.
Kwa upande wake afisa Elimu kata ya Makanda Mwalimu Musa Amana amesema shule zinafunguliwa 11/1/2021 amesema licha ya kuezuliwa kwa darasa hilo lakini kuna upungufu wa vyumba vya madarasa kwani kunaongezeko la wanafunzi 93 mwezi wa kwanza watakao anza masomo.
Kwa upande wa madawati amesema shule ina madawati 170 wakati mwezi wa kwanza wanatarajia kupokea wanafunzi 212 hivyo wanafanya kila jitihada kuhakikisha shule zinapofunguliwa wawe wamepata madawati ya kutoshereza wanafunzi hao.
Amewaomba wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhakikisha watoto katika kata hiyo wanaanza masomo katika mda mwafaka pasiwepo na visingizio kwa wanafunzi kuto ripoti shuleni.
Nae Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Makanda Mwalimu Frank Samatha amesema wakati mapaa hayo yakiezuliwa wanafunzi wote walikuwa likizo na hakuna mtu yeyeto aliyezulika kutokana na tatizo hilo.