Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Lilondo Halmashauri ya wilaya Madaba wakimsikiiza Mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Mhagama(hayupo pichani)katika mkutano wa mbunge huyo kuwashukuru wananchi hao kwa kumchagua kuwa Mbunge kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
*************************************
Na Muhidin Amri,
Madaba
WAKATI wizara ya nishati ikijivunia kusambaza umeme kwa asilimia zaidi ya 80 katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hali ni tofauti kwa wakazi wa kijiji cha Lilondo jimbo la Madaba, ambao wameliomba shirika hilo kufikisha umeme katika mtaa wanaoishi ili waweze kutumia kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayolenga kuwainua kiuchumi.
Wakitoa kilio chao mbele ya Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Mhagama wamesema, katika Utekelezaji wa mradi wa umeme kupitia mradi wa Rea awamu ya kwanza na pili, baadhi ya wananchi wamerukwa kwa kutounganishwa licha ya kulipa gharama zote zinazohitajika na kufanya maandalizi muhimu kama kufanya wayalingi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Lusitika Wella na Alex Mlelwa wamesema, umeme katika kijiji hicho umefika lakini katika mtaa wa Msekenalo na Ofisini hakuna nguzo hata moja,hivyo kuwakatisha tamaa kama na hakuna jitihada zozote za kufikishwa kwa nishati hiyo karibuni.
Lusitika Wella amesema wanahitaji sana kupata huduma hiyo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi ikiwemo kufungua salon za kike na kiume, biashara ndogo ndogo na kupata nafasi ya kuwaona vingozi wao wakitoa maagizo na kushiriki kazi za maendeleo kupitia televisheni na Radio.
Akizungumza huku akitokwa na machozi Wella amesema, kwa muda mrefu wanatamani kupatiwa umeme katika makazi yao, lakini wanakwamisha na shirika hilo ambapo amezungumzia kitendo hicho kama upendeleo kwa baadhi ya watu hasa wale wenye nguvu kubwa ya fedha.
Aidha,ameiomba wizara husika ya nishati kuingilia kati suala hilo kwani linakwamisha juhudi za Rais Dkt John Magufuri ya kuunganisha umeme kwa kila mwananchi kama mkakati wa kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi hapa nchini.
Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Mhagama amesema,vijiji 21 kati 22 vilivyopo katika jimbo la Madaba halmashauri ya madaba vimefikiwa na huduma ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini Rea awamu ya kwanza na pili.
Amesema, jimbo la Madaba ndilo lenye bahati kubwa kwa vijiji vingi kufikiwa kwa nishati ya umeme ikilinganisha na majimbo mengine ya mkoa wa Ruvuma ambao kwa kiasi kikubwa umeharakisha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Halmashauri .
Mhagama amesema, serikali imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya kufikisha umeme kila kijiji katika jimbo hilo kupitia Rea awamu ya tatu, ikiwemo kijiji cha Ifinga kata ya Matumbi km 48 kutoka kijiji cha Wino Barabara kuu ya Songea Njombe.
Amewataka wananchi wa Madaba kuwa na imani na serikali yao ya Chama cha Mapinduzi,ambayo imedhamiria kutekeleza ahadi zake kwa vitendo na kuwaomba kuiunga mkono katika kazi ya Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayokusudia kuboresha maisha ya wananchi.