Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani Peter Mollel akilaani juu ya clip iliyosambazwa ikimkashifu Waziri wa Madini na mameneja wawili wa migodi ya Tanzanite, kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Awadhi Omary na kulia ni Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani Rachel Njau.
Meneja wa mgodi wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wa Carlifornia Camp, Omary Mandari akikanusha kupanga njama za kuwahujumu wachimbaji wa madini hayo kushoto ni Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani Peter Mollel.
Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani Rachel Njau akisoma tamko la kulaani taarifa iliyosambazwa ikimkashifu Waziri Biteko.
**************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelaani vikali taarifa potofu iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuhusisha Waziri wa Madini Dotto Biteko na baadhi ya mameneja wa migodi hiyo kupanga njama za kuwahujumu wachimbaji wa madini hayo.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau akisoma tamko la wachimbaji hao amesema hivi karibuni kuna clip imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuhusisha Waziri Biteko na mameneja wawili wa migodi Omary Mandari na Saitoti Mollel kuwahujumu wachimbaji jambo ambalo halina ukweli.
“MAREMA tunajua clip hiyo siyo tuu ina lengo la kumchafua Waziri Biteko bali kudhoofisha utendaji wake kazi ili ashindwe kuwasimamia na kuwadhibiti wezi walanguzi watoroshaji wa madini ya Tanzanite wasiokuwa waaminifu wala Wazalendo wa Taifa,” amesema Njau.
Ameiomba Serikali iwasake kwa nguvu zote wote waliohusika kupanga njama hizo ovu za kumchafua Waziri Biteko ikiwemo kauli kwenye clip hiyo iweze kuwachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Amesema MAREMA wanatoa tamko la kulaani vikali dhidi ya clip hiyo kwani Waziri Biteko hana maslahi binafsi na madini ya Tanzanite na siyo kweli kuwa Mandari na Saitoti waliotajwa kwenye clip hiyo walikwenda Dodoma kuonana na Waziri ili kupanga namna ya kuwabana wachimbaji.
Amesema endapo kutakuwa na changamoto yeyote wanaomba wafikishe kwenye vyombo husika, ofisi ya mkuu wa Mkoa, Wilaya, Ofisa madini mkazi au Waziri Biteko ambaye anafikika.
“MAREMA tunakupa pole Waziri Biteko na tunakuahidi tutakuwa pamoja kupigana vita dhidi ya wezi, walanguzi na watoroshaji wa madini ya Tanzanite ili kuhakikisha yanakuwa na tija kwa Taifa letu,” amesema Njau.
Clip hiyo inamtuhumu Waziri Biteko kupanga njama na mameneja hao ili atoe agizo la watu kusachuwa migodini ili kinachopatikana wagawane kwa nyakati tofauti jambo ambalo MAREMA wamelikanusha.
Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani, Peter Mollel amesema wametoa tamko hilo la kulaani baada ya kusambaa taarifa hizo potofu kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri Biteko, Mandari na Saitoti wameandaa mpango wa kuwahujumu wachimbaji ndiyo sababu Waziri akatoa uamuzi huo kwani inachafua sekta hiyo.
Mollel amesema wao kama chama wameona ni vyema kutoa tamko la kulaani taarifa hizo potofu kwani wana imani na Waziri Biteko na wapo naye bega kwa bega katika kuhakikisha madini ya Tanzanite yanalipiwa kodi na hayatoroshwi.
Amesema Waziri Biteko ana mahusiano mazuri na wachimbaji madini hivyo kauli hiyo ya uchochezi imewaathiri wao katika sekta hiyo.
Meneja wa mgodi wa Carlifornia Camp Omary Mandari ambaye clip hiyo inamtuhumu, amekanusha vikali taarifa hizo kwa kudai kuwa huwa anajishughukisha pia na kilimo hivyo hakuna tatizo yeye kwenda Dodoma japokuwa hakuonana na Waziri Biteko.
Mandari amesema hata hivi sasa kwenye mgodi anaousimamia hapekui watu kama ilivyosemwa kwenye clip hiyo ila anasimamia kazi kama ilivyoelezwa kwenye sheria, taratibu na kanuni.
“Lengo la kuzungumzwa maneno hayo ya uzushi na kusambazwa kwa clip hiyo sijatambua ni nini ila nachofahamu hata wachimbaji wenzangu wanafahamu siwezi kuwahujumu kwa lolote,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro, Awadhi Omary amesema clip hiyo ameisikiliza kwenye gurupu la CCM Wazalendo na wala siyo kauli ya chama kwani wao wana utaratibu wa kufikisha hoja kwa njia ya vikao na siyo kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii.
Awadhi amesema ameshangazwa na kauli hiyo ya kumchafua Waziri Biteko na mameneja hao kutolewa kwenye mitandao ya kijamii na kuhususisha chama hicho.