Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Joseph Mkirikiti akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa huo (RCC) kilichofanyika mjini Babati.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau akizungumza kwenye kikao cha RCC mjini Babati.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akizungumza kwenye kikao cha RCC mjini Babati.
****************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Joseph Joseph Mkirikiti amewataka wadau wa maendeleo nchini kuwekeza kwenye Wilaya za Mkoa huo kutokana na kuwepo kwa fursa mbalimbali za kiuchumi.
Mkirikiti ameyasema hayo wakati akizungumza mjini Babati kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa huo (RCC) kilichohusisha wakuu wa wilaya, wabunge, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, makatibu tawala na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Amesema mkoa huo una fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, madini, uvuvi, utalii na nyingine hivyo ni muda wa kuchangamkia fursa hizo kwenye mkoa huo wa tatu kwa ukubwa nchini.
“Ni vizuri tukajadiliana na kila mmoja wetu akajipima ili tukauweka Mkoa wetu kuwa katika namna bora Zaidi” Alisema Mhe.Mkirikiti.
Hata hivyo, amewataka watendaji kujenga mahusiano mazuri ya kazi kati yao na wawakilishi wa wananchi ili kujua matatizo yanayoikabili jamii kwa lengo la kuwaletea maendeleo katika maeneo mbalimbali.
“Tuache kulalamika sasa ni muda wa kila mmoja kuja na mbinu za kufanikisha majawabu na kutotoa changamoto pekee, tutumie kikao hiki tujadiliane kwa uwazi, bila shaka nina Imani tukiangalia yale yaliyojadiliwa na wenzetu katika vikao vilivyopita tukaweka na dira yetu bila shaka tutafanikiwa kwa kupiga hatua zaidi,” amesema Mkirikiti.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Babati Mjini amesema bado changamoto ya bei ya maji ipo juu kwa wananchi hivyo Bawasa wahakikishe wanateremsha ankara ili iwiane na maeneo mengine wanavyolipa.
“Wananchi wa Mji mdogo wa Kiabakari Mkoani Mara wanalipa ankara ya maji shilingi 300 kwa kila uniti sisi Babati ndiyo mji pekee tunalipishwa ghali kwani kwa kila uniti tunatozwa shilingi 1,800 hapana kwa kweli, Bawasa mnapaswa kutafakari hilo,” amesema Gekul.
Mbunge wa jimbo la Kiteto, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau, amesema baadhi ya sehemu za eneo hilo kuna changamoto ya mawasiliano ya simu hivyo upatikane ufumbuzi na pia wananchi bado wanalalamikia kukatika kwa nishati ya umeme kila mara na hawapatiwi majawabu yanayojitosheleza.
“Wafanyakazi wa Tanesco wakiulizwa juu ya kukatika mara kwa mara kwa umeme, badala ya kuja na wajawabu yenye tija wanadai kuwa nishati hiyo imetoka Dodoma, utadhani Dodoma ni eneo lingine tofauti na nchi hii,” amesema Ole Lekaita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema migogoro ya ardhi pia inatakiwa kupatiwa ufumbuzi ili kero hiyo ya wananchi itatuliwe.