Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mbaraka Semwanza aliyemwakilisha Kamshina Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga (kulia), akiwa pamoja na Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza (kushoto) wakati wakusaini hati ya mashirikiano na Chama cha Skauti Tanzania, kwa lengo la kupanua wigo wa kuelimisha jamii na chama hicho kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na majanga, makubaliano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma mapema leo asubuhi. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza (kushoto) akikabidhiwa hati ya mashirikiano baada ya zoezi la kusainiwa kukamilika na Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mbaraka Semwanza, aliyemwakilisha Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga (kulia), wakati wakusaini hati ya mashirikiano na Chama cha Skauti Tanzania, kwa lengo la kupanua wigo wa kuelimisha jamii na chama hicho kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na majanga, makubaliano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma mapema leo asubuhi. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
************************************************
DODOMA, 23/12/2020
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesaini makubaliano ya kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania kwa lengo la kupanua wigo wa kuelimisha jamii na chama hicho kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na majanga, makubaliano hayo yamefanyika Jijini Dodoma mapema leo asubuhi.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Skauti Mkuu, Mwantumu Mahiza alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa wimbi la moto kwenye shule na katika jamii.
“Kazi ya chama cha Skauti ni kusaidia watu na viumbe na kuhakikisha nchi inakuwa na amani na salama kwa kuishi. Tulipoona majanga ya moto yanajitokeza kwenye shule na makazi ya watu, Skauti tukaona kuna haja ya kushirikiana na chombo cha kisheria.
“Skauti tumeshiriki kwenye mambo mengi ya Uokoaji, tulikuwa tunafanya bila kuwa na chombo cha mshikamano kisheria, mtakubaliana na mimi kuwa askari wa zimamoto walikuwa wakikutana na skauti kwenye majanga, kila mtu akifanya lake na hakuna aliyekuwa anaona umuhimu wa kumsirikisha mwenzake.”
Alisema kutokana na ushirikiano huo walioingia, sasa itakuwa rahisi kwa Jeshi la Zimamoto na Uokozi kupata taarifa pindi kunakapokuwa na viashiria vya moto kwenye shule na katika jamii.
“Kwenye shule hizi tuna wajumbe ambao ndio skauti wetu tukasema sasa umefika wakati wa kuvunja ukimya, hivyo madhumuni ya kusaini makubaliano haya kwamba sasa tunataka tufanye kazi kwa pamoja, umoja huu utasaidia kupeana maelekezo kwa sababu skauti wako katika shule na mabweni na katika makazi ya wananchi na watakapoona viashiria ni rahisi kutoa taarifa na kazi yenu itakuwa nyepesi kuanzia sasa.
Aidha, Mahiza alisema kupitia makubaliano hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji watatoa mafunzo kwa Skauti jinsi ya kukabiliana na moto na majanga mengine nao kushiriki kutoa elimu kwa jamii.
“Malengo ni kuhakikisha skauti kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji tunafanya kazi kwa pamoja kutoa elimu kuifanya nchi yetu iwe salama na wananchi wake waweze kuishi kwa amani ili waweze kutenda majukumu yao pasipo na shaka yoyote
Alisema matarajio ya chama cha skauti ni kuwa mafunzo haya yataanza kutolewa mwakani pindi shule zitakapofunguliwa.
“Tunaamini kwa idadi ya shule tulizonazo maana tuna shule 23550 zenye idadi wanafunzi wasiopungua 9,200,060, endapo kila mmoja akapata mafunzo na kufundisha watu wanne tu basi kwa muda mfupi tunaweza kufikia watu takribani milioni 36 wakati kazi hii ingefanywa na Jeshi pake yake ingekuwa ngumu.”
Naye Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mbaraka Semwanza, aliyemwakilisha Kamshina Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga, alisema Jeshi lake linaamini baada ya kuanza ushirikiano huo elimu ya Kinga na Tahadhari Dhidi ya majanga ya moto na majnga mengine itawafikia Watanzania wengi.
“Jukumu ya Jeshi letu ni Kuokoa Maisha ya Watu na Mali, na sasa Tanzania tumeingia uchumi wa kati unaojengwa na miundombinu ambayo inahitaji Ulinzi na Usalama wa moto na majanga mengine, hivyo ushirikiano huu umekuja muda muafaka.”
Alisema pia Jeshi lake litaangalia namna ya kushirikiana na Chama cha Skauti katika suala la uokoaji kutokana na tatizo la mafuriko ya mara kwa mara yanayotokea.
“Baada ya makubaliano haya natarajia tutaongeza uelewa wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto na majanga mengine kwa mtu mmoja mmoja kwa sababu watu watafikiwa, miundombinu, maisha yao yatakuwa salama. Sasa tumepata mabalozi wa kufanya nao kazi, hivyo na hakika mwaka 2021 tutaunza vizuri.”