…………………………………………………………………
Kampuni ya ZECO yapewa siku 14 kukamilisha ukarabati wab wawa la Kimokuwa litakalotumika kwa ajili ya matumizi ya kunyweshea mifugo na matumizi ya binadamu.
Maelekezo hayo yametolewa jana (22.12.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya ukarabati wa mradi huo unaotekelezwa katika kijiji cha Kimokuwa, wilayani Longido, mkoani Arusha.
Prof. Gabriel amesema mwanzoni kampuni hiyo ilianza kazi vizuri lakini mwishoni kumekuwa na tatizo kwani usimamizi wao wa mradi sio mzuri kitu ambacho kimesababisha umaliziaji wa mradi kuwa na mapungufu. Pia amemtaka mkandarasi kujiridhisha kwenye kingo za bwawa hilo walizoziweka kwani ikitokea zikabomoka hatua kali zitachukuliwa dhidi ya kampuni hiyo.
Kutokana na mapungufu aliyoyaona amempa mkandarasi siku 14 kuhakikisha anakamilisha mradi. Kutokana na kuwepo kwa mapungufu hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul hataupokea mradi huo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Prof. Gabriel amewasihi wakandarasi wazawa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa umakini ili waendelee kuheshimika na kupewa kazi na serikali kwani fedha zinazotolewa za miradi zinatoka kwa wananchi walipa kodi. Hivyo amewataka wafanye kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia viwango.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Bw. Simba amempogeza Katibu Mkuu Gabriel kwa uamuzi wake wa kukagua maendeleo ya mradi huo kabla ya kukabidhiwa kwa mapungufu yaliyopo hata uongozi wa wilaya ulishayabaini. Lakini pia amemsihi mkandarasi kuhakikisha anayafanyia kazi mapungufu yote yaliyoainishwa katika ukaguzi huo ili wafugaji na jamii kwa ujumla iweze kupata huduma hiyo ya maji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimokuwa, Bw. Kileli Olendere amesema Katibu Mkuu yupo sahihi kuamua kutomleta Naibu Waziri kuja kukabidhiwa bwawa hilo kwani ukarabati wake bado haujakamilika hivyo ni vema mkandarasi kwanza akamilishe kazi zinazotakiwa ndipo mradi ukabidhiwe kwa viongozi pamoja na wananchi.
Zephania Umbuli ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya ZECO Construction amesema ameyapokea maelekeo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Gabriel na ameahidi kuyatekeleza ndani ya siku 14 walizopewa.
Naye Kasaini Lemaiba amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuona umuhimu wa kutatua tatizo la upatikanaji wa maji kwa wafugaji kwani mifugo inamchango katika kukuza pato la taifa. Lakini pia ameahidi kuwa endepo serikali itaendelea na mipango yake ya kuboresha huduma za maji kwa wafugaji pamoja na nyanda za malisho, wafugaji hawatakuwa na sababu ya kuhama hama.
Ukarabati wa bwawa hili la Kimokuwa unaogharimu milioni 511.9 ulitakiwa kukamilika Novemba 25. 2020 lakini mkandarasi aliomba kuongezewa muda mpaka Decemba 10. 2020. Kutokana na mapungufu yaliyoainishwa amepewa siku 14 mpaka Januari 06, 2021 kuhakikisha anakamilisha kazi vinginevyo hatua za kimkataba zitaanza kuchukuliwa.