Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi ripotri ya Mradi wa ZUSP Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ZAECA Nd,Mussa Haji Alikwa, ajili ya kuifanyika kazi wakati mkutano wake na Wafanyakazi wa mamlaka hiyo leo uliofanyika Ofisi za Idara Victoria Garden Jijini Zanzibar.[Picha na Ikulu].23 Disemba 2020. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akijibu masuala ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ZAECA wakati mkutano wake na Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo leo uliofanyika Ofisi za Idara Victoria Garden Jijini Zanzibar (kushoto) Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ZAECA Nd,Mussa Haji Ali.[Picha na Ikulu].23 Disemba 2020.
Zanzibar Disemba 23, 2020
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemsimamisha kazi Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Sabra Issa Machano na watendaji wengine kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbali mbali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali.
Dk. Mwinyi ametoa kauli ya kuwasimamisha watendaji hao wakati alipozungumza na Viongozi na watendaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) katika ukumbi wa taasisi hiyo uliopo Victoria Garden, Vuga Jijini hapa.
Watendaji wengine waliohusika na hatua hiyo ni pamoja na Ramadhani Abdalla Ali pamoja na watendaji wa Kamati nzima ya Uratibu wa mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kutoka Wizara ya Fedha.
Alisema amechukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF Sabra Issa Machano pamoja Ramadhani Abdalla Ali kwa makosa ya kiutendaji katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Jumba la Treni liliopo Darajani.
Alisema ni dhahiri kuwa katika utekelezaji wa mradi huo taratibu zilikiukwa na hivyo akabinisha ulazima wa kufanyika uchunguzi, wakati ambapo watendaji hao wakiwa nje ya kazi.
Alisema makosa dhidi yao hayatoi fursa ya wao kuendelea na kazi , hivyo ni vyema wakae pembeni kupisha uchunguzi na kusema Serikali itasimamia haki na kamwe hakuna mfanyakazi atakaeonewa dhidi ya tuhuma zinazowakabili.
Aidha, alisema hafurahishwi na utekelezaji wa mradi wa ZUSP uliogharimu Dola Milioni 93, ambao ulikusudiwa kuondoa changamoto mbali mbali katika Manispaa.
Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwepo makosa makubwa katika manunuzi pamoja na kufanyika udanganyifu juu ya kazi zilizoelezwa kufanyika, il-hali hazikufanyika.
Alisema amelazimika kuisimamisha Kamati nzima ya Uratibu wa Mradi huo ili uchunguzi uweze kufanyika, wakati wafanyakzi hao wakiwa nje ya kazi zao.
Vile vile Dk. Mwinyi aliagiza ZAECA kufanya Uchunguzi wa kina dhidi ya Mfanyakazi wa TRA Haidar Mussa Maisara anaetuhumiwa kushusha kiwango cha kodi katika tukio la kuingizwa Bandarini kichwa cha Scania, sambamba na Kampuni ya KEVIS aliyoaguiza ifanyiwe uchunguzi.
Alisema mfanyakazi huyo alijenga dhamira ya kujihusisha na rushwa, ambapo kwa nyakati tofauti aliteremsha kiwango cha kodi hiyo hadi kufikia shilingi Milioni tano, fedha ambazo haziendani na thamani halisi ya kodi iliyopaswa kulipwa, ambapo hatimae gari hilo lilitolewa usiku bila fedha hizo kulipwa.
Alisema anasikitishwa na miradi mikubwa jinsi ilivyogubikwa na matatizo makubwa kiasi ambacho haionyeshi thamani ya fedha zilizotumika na hivyo akaahidi kuchukua hatua mara moja dhid ay wote waliokiuka kanuni z amanunuzi.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi alisema tangu Serikali ya Awamu ya nane iingie madarakani imebaini kuwepo matatizo makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, na hivyo akasisitiza dhamira ya Serikali ya kuchukua hatua madhubuti.
Aidha, alisema kuna miradi mingine inayoonesha dalili za kuwepo mianya ya rushwa na hivyo akaahidi kuifuatilia pamoja na kuhakikishia ZAECA kuwa serikali imefungua ukurasa mpya wa mapambano dhidi ya rushwa.
Mapema Waziri wa Nchi (OR) Katiba, sheria, utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema kuna mashirikiano makubwa ya kiutendaji kati ya ZAECA na wenzao wa Tanzania Bara (TAKUKURU) kutokana na vikao mbali mbali vilivyofanyika, na hivyo akaahidi kuendeleza mshirikiano hayo kwa lengo la kudumisha Muungano.
Alisema akiwa Kiongozi wa Wizara, atasimamia kikamilifu kuona matukio ya rushwa na udhalilishaji yanamalizika kabisa hapa nchini.
Nae, Mkurugenzi Mkuu ZAECa Mussa Haji Ali alisema pamoja na taasisi hiyo kuasisiwa katika kipindi kifupi kilichopita, imeweza kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake makuu matatu.
Akigusia uchunguzi wa miradi mikubwa inayotokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya serikali, alisema ZAECA inaendelea kufanya uchunguzi katika miradi mbali mbali ikiwemo wa Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri na ukarabati wa jengo la Treni ambayo imebainika kuwepo harufu za rushwa.
Alisema miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi ni Barabara ya Bububu – Mkokotoni Kaskazini Unguja pamoja na ile ya Ole – Kengeja inayoonekana kuwepo harufu ya rushwa katika suala la tathmini.
Aidha, aliitaja miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi kwa tuhma za kuwepo mianya ya rushwa, kuwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Amali Vitongoji, Bandari ya Mangapwani, Soko la Matunda Kangani, Ujenzi wa kiwanda cha ushoni cha Idara Maalum, mradi wa kuendeleza vijana, ujenzi wa vituo vya Zimamoto Pemba, Kuimarisha majengo ya JKU Mtoni, Matengenezo kambi ya KVZ Pemba pamoja Chuo cha Mafunzo Wete.
Alieleza kuwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya nane, wananchi wamekuwa na imani kubwa na Serikali na hivyo wamekuwa wakisaidia katika utoaji wa taarifa.
Alimhakikishia Rais kuwa taasisi hiyo ina mashirikiano mazuri na taasisi za ndani na nje ya nchi pamoja na vyombo vyote vya uchunguzi,, ikiwemo TAKUKURU.
Akigusia changamoto, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa jengo lemye hadhi pamoja na kuwa na muundo usiowakurubisha wananchi na hivyo kuwa na tatizo katika upokeaji wa taarifa katika Wilaya na Mikoa.
Aidha, alisema taasisi inakabailiwa na chanagmoto ya vifaa mbali mbali vya utendaji pamoja na mafunzo kwa watendaji,.