***********************************************
NJOMBE
Waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Seleman Jafo ametoa agizo kwa wakurugenzi wa mamlaka zote 185 za halmashauri nchini ifikapo desemba 30 kuhakikishe wanafika asilimia 50 ya makusanyo ya nusu mwaka ya mapato waliyokuwa wamepitisha katika bajeti vinginevyo watakuwa katika wakati mgumu wa kuendelea kutumikia nafasi zao
Jafo ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya mji wa Njombe ambapo amesema kumekuwa na uzembe mkubwa wa upotevu wa mapato kwa halmashauri nyingi jambo ambalo linapelekea serikali kushindwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa wakati.
Akieleza mwenendo wa makusanyo kwa halmashauri za mkoa wa Njombe amesema hadi sasa halmashauri ya wilaya ya Njombe ndiyo kinara kwa makusanyo ambapo imekusanya asilimia 72, ikifuatiwa na halmashauri ya mji wa Njombe iliyokusanya asilimia 48 katika kipindi cha miezi 6 huku akiinyoshea kidole halmashauri ya wilaya ya Makete ambayo bado ipo kwenye asilimia 20 ya makusanyo hadi sasa.
Mafanikio ya makusanyo yaliopigwa katika halmashauri ya wilaya ya Njombe na Njombe Mji yamekisukuma kituo hiki kuzungumza na Ally Juma mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya na Illuminata Mwenda mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe ambao wanasema hatua hiyo ni mafanikio ya ubunifu wa vyanzo vya mapato na kuziba myanya ya utoroshaji mapato.
Mbali na Kuongea na Watumishi waziri Jafo pia amekagua ujenzi wa mradi wa kituo cha afya Kifanya kinachojengwa kwa mapato ya ndani na halmashauri ya mji wa Njombe kikitazamiwa kugharimu zaidi ya mil 395 na kisha kuahidi kupeleka vifaa na dawa punde kitakapokamilika .