Mtaalam na Msimamizi wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Alex Njahani akizungumza na waandishi wa habari namna program hiyo inavyochangia mabadiliko ya maisha kwenye vijiji vya mradi.
Mratibu wa Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Emmanuel Msoffe akiandaa mche wa Msaji mbele ya waandishi ili ukapandwe.
………………………………………………………………………..
NA SULEIMAN MSUYA
WATANZANIA wameshauriwa kutunza na kuendeleza rasilima misitu ili kuwa na uhakika wa kupata mvua na kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Aidha wameshauriwa kupanda miti aina ya misaji ambayo inafaa kibiashara huku wakijihusisha na shughuli nyingine za kujipatia kipato.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa Program ya Myororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) Emmanuel Msoffe wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Liuli na Nkalachi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ambao wanatekeleza mradi wa upandaji miti ya misaji kijijini hapo.
Msoffe aliambatana na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kujionea namna miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) inavyotelezwa kwenye vijiji ambapo ziara ilianzia mkoani Lindi na kuishia wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Amesema program ya FORVAC inatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki chini ya ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland na Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania.
Tanzania ina hekta milioni 48.1 za misitu lakini kutokana na ukataji miti hekta 469,000 zinaisha kwa kukatwa kila mwaka.
Msoffe amewataka wananchi wenye misitu ya asili popote Tanzania kuitunza huku wakiendelea na upandaji wa miti.
“Hapa Liuli mmeonesha mfano wa kuendeleza misitu kwa kutunza Mlima Livingston lakini niwapongeze kwa kuamua kupanda miti ya misaji ambayo ni fursa kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Mratibu amesema uhakika wa kuwepo misitu utakuwa endelevu kwa wanavijiji kuendelea kupanda miti ya kibiashara kama misaji inayokubali eneo hilo.
Amesema utafiti wao umebaini kuwepo kwa mapungufu ya kiusimamizi ndio sababu ya uharibifu wa misitu hivyo kuishauri Serikali kutafuta na kutumia fursa zilizopo.
Ameitaka jamii kuondokana na hofu ya muda mrefu wa kusubiria kuvuna bali wajionee huruma kwa sasa kurudi mabadiliko ya tabia nchi.
Mratibu huyo amesema wataendelea kuhamasisha jamii umuhimu wa kutunza misitu na vyanzo vya maji.
Kwa upamde wake Msimamizi wa Mtaalam wa Misitu wa FORVAC, Alex Njahani amesema uendelevu wa misitu ya vijiji na ile ya Serikali utachangiwa na ushirikiano wa wadau wote.
Njahani amesema program hiyo imeweza kutoa matoe chanya kwa Semina elekezi kwa vikundi ambavyo vinajihusisha na lengo husika.
“Sisi tumekuwa tunashirikiana na wadau kuhakikisha sekta ya misitu inakuwa na tija kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa,” amesema.
Mtaalam huyo amesema FORVAC inatekeleza program hiyo kwenye wilaya 12 ambazo ni Nyasa, Mbinga, Namtumbo, Songea na Tunduru zilizopo Kongani ya Ruvuma.
Amesema wilaya zingine ni Liwale, Ruangwa, Nachingwea Kongani ya Lindi, Handeni, Kilindi, Mpwapwa na Kiteto Kongani ya Tanga.
Njahani amesema matarajio yao ni kuona wanavijiji wanaozungukwa na misitu ya vijiji wananufaika nayo kupitia dhana ya USMJ.