******************************************
Wakulima wa mazao ya mbogamboga na matunda ikiwemo vitungu na nyanya Mkoani Morogoro wamehimizwa kuanza kufanya mapinduzi ya kilimo badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea ili kukidhi vigezo vya masoko ya Kimataifa vitakavyowezesha mazao hayo kuuzwa nje ya nchi.
Akizungumza na Wananchi wa Idete na Lumuma Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro,Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kilosa ametoa rai hiyo kwa wananchi hao kutokana na wananchi hao kutumia nguvu kubwa kulima na kupata mazao ya kutosha lakini hawanufaiki na jasho lao kutokana na mazao mengi kuoza kabla ya kumfikia mlaji
Prof. kabudi amesema kuwa wakati umefika sasa wa kufanyika utafiti wa kutosha juu ya aina ya vitunguu na nyanya zinazolimwa mkoani humo jambo litakalowezesha kupata mbegu bora ambazo zinadumu kwa muda mrefu hususani wakati wa kusafirisha mazao baada ya kuvuna mpaka kumfikia mlaji bila kuharibika kama ilivyo sasa.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli imefanya ununuzi wa ndege maalum kwa ajili ya kubeba mizigo kupeleka nje ya nchi na kubainisha kuwa ilani ya chama cha mapinduzi CCM inamtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Mabalozi wote kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali za kilimo zinazolimwa hapa nchini kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi kwa kutumia ndege za shirika la Tanzania.
Baadhi ya wakulima wa vitunguu na nyanya katika maeneo hayo ya Lumuma na Idete wameiomba Serikali kuhakikisha pembejeo za Kilimo zinawafikia moja kwa moja badala ya kupitia kwa mawakala ambao huzipandisha bei maradufu na kuwafanya wakulima kutonufaika na matunda ya kilimo baada ya mavuno kwa kubakia na madeni