Askofu msaidizi wa Kanisa Katoliki Arusha mhashamu Prosper Lyimo (kulia) akiongoza misa ya harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mirerani, wapili kulia ni mgeni rasmi wa harambee hiyo mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka na Paroko wa Parokia hiyo Vincent Ole Tendeu, kulia ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Siria Meibuko ambapo zilizopatikana shilingi milioni 50 zilipatikana.
Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, mhashamu Prosper Lyimo (kulia) akiweka wakfu Kanisa jipya la Parokia ya Mirerani, ambapo mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka (kushoto) aliongoza harambee na kupatikana shilingi milioni 50.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka (mwenye suti nyeusi) akiingia kwenye harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mirerani, ambapo shilingi milioni 50 zilipatikan.
……………………………………………………………………..
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole SENDEKA amesema kauli ya Waziri wa Madini Dotto Biteko imelenga kudhibiti utoroshaji wa madini na siyo kuzuia wachimbaji wadogo wa madini kuwa na Tanzanite.
Hivi katibuni, Waziri Biteko alitoa agizo la kufuta leseni kwa wamiliki wa migodi ya Tanzanite na madalali watakaobainika kushiriki utoroshaji wa madini ya Tanzanite na udanganyifu.
Hata hivyo, wachimbaji hao wadogo wanatakiwa kuuza madini hayo ndani ya ukuta au kupita nayo lango la ukuta baada ya kulipa kodi kuliko kuyapitisha kwa wizi na kuingia hatiani.
Ole Sendeka aliyasema hayo wakati akiongoza harambee ya ujenzi wa kanisa katoliki, jipya la Mji mdogo wa Mirerani, ambapo zilipatikana shilingi milioni 50 ikiwemo fedha taslimu na ahadi.
Alisema kauli ya Waziri Biteko imetafsiriwa tofauti kwani wanaApolo ndiyo nguvu kazi ya uchimbaji na hawalipwi mishahara hivyo wanapaswa kupata mgao kupitia madini.
Alisema baadhi ya wadau wa madini hawakuelewa agizo la Waziri Biteko ndiyo sababu imesababisha sintofahamu juu ya maslahi ya wanaApolo.
“Lengo ni kuhakikisha kutowepo na wizi wa madini au udanganyifu ila maslahi ya wanaApolo lazima yaangaliwe kwani wao ndiyo nguvu kazi na bila hivyo shughuli hazitafanyika,” alisema Ole Sendeka.
Alisema ni vyema wamiliki wa migodi wakae kwa pamoja na kuzungumza na wanaApolo ili wafahamu hatima yao juu ya maslahi ili kuondokana na sintofahamu iliyopo hivi sasa.
Askofu msaidizi wa jimbo kuu Katoliki Arusha, mhashamu Prosper Lyimo, akizungumza kwenye harambee hiyo aliwashukuru wote waliojitolea kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.
Askofu Lyimo alisema pindi watu wakutanapo hata chini ya mti kwa lengo la kusali, kumuomba na kumshukuru Mungu hilo ni kanisa, hivyo anawapongeza waamini kwa kujitolea ujenzi huo.
“Nawashukuru wote kuanzia mgeni rasmi Ole Sendeka, waamini wote, jumuiya zote, vyama vya kitume na wadau wote wa maendeleo waliojitolea kwa ajili ya ujenzi wa kanisa,” alisema.
Awali, katibu wa kamati ya ujenzi wa kanisa hilo Raphael Ombade alisema gharama zitakazotumika kwenye ujenzi huo ni shilingi milioni 900.
Ombade alisema ujenzi wa kanisa hilo utajengwa kwa awamu nne ikiwemo msingi, ukuta, upauzi na kisha umaliziaji.