*****************************************
Kuelekea sikukuu ya Krismas, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kikamilifu kusimamia usalama katika kipindi chote cha sherehe za sikukuu ya Krismas kwa kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika katika hali ya Amani na Utulivu.
Mkoa wetu unapakana na nchi jirani ya Malawi [Kasumulu Border] kwa upande wa magharibi hivyo tumejipanga kuimarisha ulinzi na kuendelea kudhibiti uhalifu katika vipenyo vyote [njia zisizo rasmi] hasa biashara za magendo, ni rai ya Jeshi la Polisi kwa wakazi wa maeneo hayo kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kuelekea kipindi hiki cha sikukuu, waumini wa madhehebu ya kikristu ushiriki katika Misa za Krismas kulingana na ratiba iliyopangwa katika makanisa. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa viongozi katika makanisa kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri hasa katika suala la ulinzi kwa kutumia kamati za ulinzi na usalama zilizopo ili kuhakikisha hali ya usalama katika maeneo ya ndani na nje ya makanisa unakuwepo.
Aidha tumejipanga vizuri katika kuhakikisha watumiaji wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara wanafuata na kutii sheria za usalama barabarani katika maeneo yote. Pia katika kipindi hiki cha sikukuu tutaendelea na utaratibu wetu wa kupitisha magari kwa awamu katika maeneo yenye milima na miteremko mikali kama vile Mlima Nyoka, Iwambi, Mwansekwa, Igawilo na Kanyegele @ Uwanja wa Ndege kule Wilaya ya Rungwe.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe na maeneo ya fukwe kule Matema Wilayani Kyela.
Hakutakuwa na Disco Toto, hivyo tunawataka wazazi na walezi kuendelea kuwalinda watoto kwa kuwaepusha na mazingira yasiyo salama kwao. Tunawataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa mtoto, na pia kuwaepusha watoto na matembezi au safari zisizo kuwa za lazima, mikusanyiko isiyo kuwa ya lazima ili kuepuka watoto kupotea katika msimu wa sikukuu.
Ninasisitiza ulinzi na usalama katika makazi yetu, kuhakikisha kwa wale wanaotoka kwenda kanisani kwa ajili ya Misa za mkesha au asubuhi kuhakikisha wanaacha waangalizi katika makazi yao. Pia ninawakumbusha kuwa ulinzi unaanza na mimi, wewe na sisi sote hivyo tuhakikishe tunajilinda kwa kufunga milango na madirisha ili kuepuka uhalifu katika nyumba zetu, watendaji wa Mitaa, Kata na Tarafa washirikiane na vikundi vya ulinzi shirikishi, Polisi Kata waliopo katika maeneo yao ili kuimarisha Ulinzi na Usalama.
Aidha nasisitiza utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kupitia namba za simu zifuatazo:-
RPC……………………………………………………………0715 009 931
OPERATION OFFICER………………………………………0737 792 510
RCO……………………………………………………………0658 376 052
RTO……………………………………………………………0658 376 472
OCD MBEYA…………………………………………………0659 884 996
OCD MBALIZI………………………………………………..0655 248 381
OCD CHUNYA………………………………………………..0659 885 384
OCD MBARALI……………………………………………….0659 885 948
OCD RUNGWE……………………………………………….0659 885 253
OCD KYELA………………………………………………….0659 887 919