Mmoja wa walimu wa darasa la Jifunze akiwafundisha wanafunzi wake darasani, ikiwa ni mradi wa majaribio unaoendeshwa na Uwezo Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ludewa.
Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Ludewa, Bw. Florian Mtweve akizungumza na mwandishi wa habari hizi(hayupo pichani). |
Wanafunzi wa darasa la Jifunze wakishangilia na walimu wao baada ya kumaliza kipindi chao. Darasa hili ni moja ya darasa la majaribio linaloendeshwa Shule ya Msingi Maholong’wa. |
Na Joachim Mushi,
Ludewa
HALMASHAURI ya Wilaya
ya Ludewa Mkoa wa Njombe inafanya utaratibu wa kutaka kuutumia mradi wa darasa
Jifunze katika shule zake zote ikiwa ni kujaribu kutokomeza idadi ya watoto
wasiojua kusoma na kuandika kuanzia darasa la tatu hadi la sita.
Taarifa zinaonesha shule nyingi za msingi katika halmashauri
hiyo zimekuwa zikiongoza ukilinganisha na maeneo mengine ya mkoa huo kwa kuwa
na idadi kubwa ya wanafunzi wasiomudu kusoma na kuandika kuanzia darasa la tatu
hadi la sita, jambo ambalo lilisababisha Taasisi ya Uwezo kutambulisha mradi wa
darasa Jifunze ambao umetekelezwa kwa majaribio katika shule tano eneo hilo
kujaribu kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Mjini
Ludewa Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Ludewa, Bw. Florian Mtweve
alisema baada ya kuona mradi wa darasa la Jifunze umepata mafanikio katika
kipindi cha majaribio kwa baadhi ya shule wanafanya mazungumzo na wakufunzi wa
Uwezo ili washirikiane kuwaandaa walimu wa serikali kwa gharama za halmashauri
kuendesha mpango huo.
“..Tunampango wa kuomba wataalam wa Uwezo wa tatu au wanne
ambao tutawaunganisha na walimu ambao tayari walipewa mafunzo ya namna ya
kuendesha darasa la Jifunze, pamoja na viongozi wa wilaya tuwafundishe walimu wote
wa shule zetu za msingi za Serikali ambazo ni 113, tuwafundishe kwa siku tatu
hadi tano ili walimu wetu waweze kufundisha kwa mfumo huo katika shule zote za
halmashauri,” alisema Bw. Mtweve.
Alisema mpango wao ni kuhakikisha wanakamilisha kutoa
mafunzo kwa walimu wao mwezi wa Desemba, ili kati ya mwezi Januari na Februari
2021 aina hiyo ya ufundishaji iweze kutumika kwa madarasa ya awali, darasa la
kwanza na darasa la pili. “…lengo letu ni mfumo huu wa darasa la Jifunze
tuuhamishie kwenye shule zetu zote za serikali, maana tumeona mafanikio yake,”
alisisitiza mkaguzi huyo wa ubora wa elimu.
Aidha alisema mradi huo maalum wa darasa la Jifunze
unaotekelezwa katika Shule tano za Msingi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya
Ludewa kwa majaribio ulio kuwa na lengo
la kuwasaidia wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wa kuanzia darasa la tatu
hadi la sita umeonekana kuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi tangu
kuanzishwa kwake na Taasisi ya Uwezo Tanzania.
Alibainisha kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo
yanaridhisha kwa kiasi kikubwa kwani ukitolea mfano tu kwa Shule tatu
zinazofanyiwa majaribio, kati ya wanafunzi 231 ambao walibainika hawajui kusoma
na kuandika kwa shuleza msingi Maholong’wa, Shaurimoyo na Matika ndani ya siku
30 baada ya kutekelezwa mradi huo ni wanafunzi 30 tu ndio walisalia hawajui
kusoma na kuandika.
Mradi wa Jifunze unaoendeshwa kusaidia wanafunzi wasiojua
kusoma na kuandika kwa darasa la tatu hadi la Sita umekuwa ukitekelezwa kwa
baadhi ya wilaya zenye changamoto ya ujifunzaji kwa wanafunzi, na umekuwa
ukiwatumia walimu waliopata mafunzo kufundisha kwa muda wa ziada kuwasaidia
wanafunzi wenye changamoto hiyo, ukitekelezwa kwa siku 30, kabla ya kufanya
tathmini kila baada ya siku 10.
Mradi umekuwa ukitekelezwa kwa walimu kutoa mada kwa vitendo
na ukaribu zaidi na wanafunzi, kujenga urafiki, kutumia vifaa rahisi
kufundishia, kuimba na kucheza na kutoa motisha kwa wanafunzi wanaojifunza
jambo ambalo limekuwa na mabadiliko makubwa katika kujifunza kwa wanafunzi eneo
hilo.