Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akizungumza na Bodi ya Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) pamoja na Menejimenti katika ukumbi wa DUWASA jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) Prof. Idrissa Mshoro (kushoto kwake) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa DUWASA jijini Dodoma.
……………………………………………………………………………………………
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameitaka Bodi ya Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) pamoja na Menejimenti yake kuanisha miradi yote ya maji vijijini yenye changamoto na kujua gharama zake na namna ya kutatua changamoto hizo.
Waziri Aweso ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Bodi ya RUWASA pamoja na Menejimenti katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.
Amewataka ifikapo mwezi Machi 2021 miradi yote yenye chagamoto iwe imefanyiwa kazi na kukamilika kwa kutoa huduma kwa wananchi yenye uhakika. Aidha, amewataka RUWASA kuongeza ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.
“Hakikisheni mnafanya kazi kwa kushirikiana kama timu moja ya Wizara ya Maji ili tuweze kutekeleza lengo letu la kuwahudumia watanzania na kuwapatia majisafi, salama na yenye kutosheleza”, Waziri Aweso amesema na kuwataka RUWASA waimarishe ushirikiano na Chuo cha Maji kwa kuwatumia wataalam wanaotoka katika chuo hicho katika usimamizi wa miradi ya maji wanayoitekeleza.
Pamoja na hilo, Mhe. Aweso ameutaka uongozi wa RUWASA kuainisha miradi yote iliyokamilika kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account) na kuhakikisha miradi yote ya maji nchini inakuwa endelevu kwa kuunda vyombo vya watumia maji vyenye uwezo wa kusimamia na kuendesha miradi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amesema moja ya changamoto inayowakabili ni rasilimali watu ambapo bado wakala huo unahitaji wataalam.
Mhandisi Kivegalo amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021 RUWASA imepanga kutekeleza miradi 1,629 na mpaka robo ya kwanza ya mwaka idadi ya miradi iliyokamilishwa ni 222.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA Prof. Idrissa Mshoro ameishukuru serikali kwa kuiwezesha RUWASA kwa namna mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake na kumhakikishia Mh. Waziri Aweso kuwa RUWASA itahakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Pia, amesema Bodi imeielekeza RUWASA kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account) ili miradi ikamilike kwa wakati na wananchi waweze kupata huduma hiyo mapema zaidi.