Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kukagua maendeleo ya uchimbwaji visima katika eneo la Mamba pembezoni mwa jiji la Dodoma, uchimbwaji wa visima hivyo ni jitihada za Serikali kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya kushitukiza ya Waziri wa Maji kukagua maendeleo ya uchimbwaji wa visima katika eneo la Mamba pembezoni mwa jiji la Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Josephat Maganga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya kushitukiza ya Waziri wa Maji kukagua maendeleo ya uchimbwaji visima vya maji katika maeneo la Mamba pembezoni mwa jiji la Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya kushitukiza ya Waziri wa Maji kukagua maendeleo ya uchimbwaji wa visima vya maji pembezoni mwa jiji la Dodoma.
…………………………………………………………………………
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amefanya ziara ya kushtukiza usiku kukagua zoezi la uchimbaji wa visima vya maji pembezoni mwa jiji la Dodoma alivyoagiza kuchimbwa ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika jiji la Dodoma.
Akizungumza akiwa kwenye mradi huo Mheshimiwa Aweso amesema ameamua kufanya ziara hiyo kuona kama agizo lake la uchimbwaji visima usiku na mchana kama linatekelezwa.
“Sote tunatambua tuna upungufu wa maji katika jiji letu na katika ziara yangu na Katibu Mkuu katika Mamlaka ya DUWASA niliagiza kuchimbwa kwa visima vya dharura na vichimbwe usiku na mchana, nimekuja kuona hilo nashukuru zoezi linaenda vizuri” amesema Mhe Aweso.
Aidha amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya maji Mhandisi Antony Sanga kuhakikisha anasimamia zoezi hilo sambamba na kuongeza uchimbwaji visima vingine viwili ili kufikia idadi ya visima vitatu kupunguza tatizo la maji katika Jiji.
Pia ameitaka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mkoa wa Dodoma DUWASA kuhakikisha wanasimamia vyema mgawanyo wa maji kwa wananchi kwamba licha ya upungufu wa maji lakini kila mwananchi ni lazima apate sababu ndio uhai wa binadamu.
Amesema Serikali inampango kabambe wa kuhakikisha inatatua tatizo la maji katika Mkoa wa Dodoma ambapo tayari wamelipa fidia tayari kwa ujenzi wa bwawa kubwa la Farukwa litakalokuwa kama chanzo cha maji na wapo katika taratibu za kufikisha maji yanayotoka ziwa Victoria.
Aidha ametoa onyo kali kwa wataalamu wa maji katika Wizara, Mamlaka za Maji na Halmashauri kuwa mda wa janjajanja umekwisha yeyote atachukuliwa hatua atakapoonekana kizembea kwenye nafasi yake kwani ilani ya chama inaonyesha wananchi wanatakiwa kupata huduma ya maji.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Mkoa wa Dodoma Mhandisi Aron Joseph amesema kisima hicho kina urefu wa mita 150 na sasa mkandarasi amefikia urefu wa mita 40 na kinatakiwa kukamilika ndani ya siku 30.
Amesema kwa sasa Jiji la Dodoma kutokana na ongezeko la watu kunahitaji mita za ujazo 103000 lakini zinazozalishwa kwa sasa ni mita ya ujazo elfu 66 hivyo jitihada kubwa zinahitajika kumaliza tatizo la maji katika jiji la Dodoma.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga amesema wizara tayari imetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya uchimbwaji wa visima pembezoni mwa jiji la Dodoma ili kukabiliana na tatizo la maji.
Amesema kisima hicho ni kikubwa kina milimita 400 ambazo ni sawa na nchi 16 na kitawekewa pampu kubwa ya kupampu maji huku akibainisha kuwa kama Wizara watatenga fedha nyingine kwa ajili ya kuongezwa kwa visima vingine viwili katika eneo hilo.