Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda wakikagua mitambo ya kuhifadhia kumbukumbu wakati walipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakiwa katika ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam tarehe 21 Disemba 2020.
************************************************
Na Mathias Canal, Wizara ya Katiba na Sheria-Dar es salam
Serikali imeutaka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wenye maskani yake Jijini Dar es salaam kuanza mchakato wa haraka kuhakikisha unahamia Jijini Dodoma.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba tarehe 21 Disemba 2020 wakati akizungumza na watumishi wa taasisi hiyo akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.
Waziri Mwigulu amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ametoa maelekezo ya serikali kuhamia Jijini Dodoma hivyo taasisi zote zinapaswa kuhamia haraka iwezekanavyo.
“Bahati nzuri mmeniambia kuwa mna kiwanja Jijini Dodoma hivyo safari ya Dodoma inawahusu ni lazima mhamie Dodoma, zile Taasisi zinazochelewa kuhamia Dodoma itafikia wakati tutafanya uamuzi wa kuziuza mkiwa ndani ya ofisi” Amekaririwa Dkt Mwigulu
Waziri Mwigulu amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RITA pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kuhakikisha kuwa wanaweka mkazo kuhakikisha taasisi hiyo inahamia Dodoma haraka iwezekanavyo.
Ameongeza kuwa Rais Magufuli ameonyesha mfano kwa kujenga Ikulu ya Chamwino inayofanana na Ikulu ya Jijini Dar es salaam huku tayari akiwa amehamia Jijini Dodoma hivyo taasisi hiyo ni muhimu kuhamia Dodoma.
“Binafsi sitopenda ikifanyika sensa ya Taasisi ambazo zinastahili kuhamia Dodoma halafu zikutwe bado zipo Jijini Dar es salaam zikiwemo taasisi za Wizara ya Katiba na Sheria”
Kadhalika ameagiza kuhakikisha kuwa watendaji wa taasisi ya RITA wanatembelea mara kwa mara Jijini Dodoma katika shughuli za kikazi ili kuendelea kuzoea Jiji hilo wakati wanafanya maandalizi ya kuhama.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda ameitaka taasisi hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kurahisisha utendaji kazi kadhalika kuongeza uwezekano wa kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari.
Pinda ameongeza kuwa serikali imekusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hivyo RITA inapaswa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma hususani katika utoaji wa vitambulisho kwa ngazi ya majimbo.
Awali akitoa taarifa ya Taasisi hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson amesema kuwa taasisi hiyo ipo katika mpango mkakati wa kuharakisha ufungaji wa mirasi kwa wakati pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuhakikisha sheria ya ufilisi inakamilika na kupitishwa na bunge.
Sambamba na hayo amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikumba taasisi hiyo ikiwemo kushindwa kuongeza ada ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na upungufu wa watumishi kwani waliopo ni 203 kati ya 361 wanaohitajika.
MWISHO