*********************************************
Na Mwandishi Wetu Kaliua
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Festo Dugange amewahimiza watendaji wa Halmashauri ya Kaliua kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani ya halmashauri ili kuwezesha uwekezaji na utoaji huduma kwa wananchi kwa ufanisi unaostahili.
Dkt. Dugange ametoa wito huo mwishoni mwa juma lililopita wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa kwenye Halmashauri za Kaliua na Urambo.
“Halmashauri zikikusanya mapato kwa ufanisi na kuwekeza kwenye huduma za kimkakati, zinasaidia kuipunguzia mzigo serikali kuu na kupunguza utegemezi wa kibajeti kwa wadau wa maendeleo”, amesisitiza Dkt. Dugange.
Akizungumza Dkt. D kuvuka malengo ya makusanyo ya mapato katika kipindi cha miezi sita kitakachoishia 31 Desemba 2020 ambapo jumla ya mkusanyo mpaka sasa imefikia asilimia 62.
Aidha katika ziara hiyo Dkt. Dugange amekagua hospitali ya halmshauri ya Kaliua, kituo cha afya Kaliua na kituo cha afya Usoke Mlimani kilichopo wilaya ya Urambo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kaliua Abel Busalama ameeleza kuwa asilimia 60% ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha 2020/2021 yaliyokusanywa mpaka sasa yameelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi wilayani humo ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya na utoaji wa mikopo kwa wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu.
Naye Mbunge wa Kaliua, Bi. Aloyce Kwezi ameomba serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya Kaliua kwa wakati ili itoe huduma tarajiwa kwa wananchi ambao kwa sasa wanalazimika kufuata huduma hiyo wilayani Urambo.