Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mkutano uliowakutanisha Makampuni manne toka China, Balozi wa Tanzania Nchini China, wadau wa kilimo na Sekta binafsi walipokutana kuzungumzia soko la zao la Soya, mkutano uliofanyika Jijini Dodoma kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe akiwasikiliza wamiliki wawili wa makampuni ya ununuzi wa Soya hapa nchini mkutano uliowakutanisha Makampuni manne toka China, Balozi wa Tanzania Nchini China, wadau wa kilimo na Sekta binafsi walipokutana kuzungumzia soko la zao la Soya, mkutano uliofanyika Jijini Dodoma njia ya mtandao.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao Wizara ya Kilimo Nyasebwa chimago akizungumza wakati wa mkutano uliowakutanisha Makampuni manne toka China, Balozi wa Tanzania Nchini China, wadau wa kilimo na Sekta binafsi walipokutana kuzungumzia soko la zao la Soya, mkutano uliofanyika Jijini Dodoma kwa njia ya mtandao.
***********************************************
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Nchini China wamefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao (Video Call) na Makampuni manne ya Nchini China kwa ajili ya kununua zao la Soya hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo ulioshirikisha Ubalozi wa Tanzania nchini China, wadau wa kilimo na Sekta binafsi Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema lengo la mkutano huo ni jitihada za Serikali kutafuta masoko ya mazao yanayozalishwa hapa nchini.
“Tumekuwa na mkutano kwa njia ya mtandao na tumefanya mazungumzo na makampuni manne kutoka China ambayo yameonyesha nia ya kutaka mazao hayo ya Soya” amesema Mhe. Bashe.
Amesema kuna makampuni manne kutoka China yameonesha nia ya kutaka kununua zao hilo hapa nchini ambalo linahitajika kwa kiwango kikubwa sana China na kutaka kupata makampuni ya ndani yatakayokuwa na uwezo wa kununua hapa nchini na kupeleka China.
Ambapo ameziagiza mamlaka husika kuanza mchakato wa kuyapata makampuni hayo yatakayoweza kukusanya zao la Soya hapa nchini na kupeleka Nchini China.
“Tunataka usajili huu usichukue mda mrefu ili tusajili kampuni hizo ili ziingie katika kanzi data ya wafanyabiashara nchini China tayari kwa kuanza kusafirisha zao la Soya” amesema.
Ametoa siku kumi na nne (14) Kuwa makampuni yote yatakayokuwa tayari kutaka kukusanya mazao kwa wakulima ili makampuni hayo yakabidhiwe kwa ubalozi wa China tayari kwa kuanza mchakato.
Amebainisha kuwa katika mazungumzo hayo ameyaambia makampuni hayo kuwa yatoe kadilio la kiasi cha tani wanazohitaji kutoka hapa nchini na kiwango cha ubora wake, bei na mda wakununua zao hilo hapa nchini.
Amesema kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania China wapo katika mchakato wa kufanya mazungumzo na Mamlaka za China kwa ajili ya kuweka matangazo ya mazao yote yanayopatikana hapa nchini kwenye miji mikubwa na ubora wake ili kupata masoko sababu china ndio soko kubwa la mazao Duniani kutokana na idadi ya watu katika nchi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao Wizara ya Kilimo Nyasebwa chimago amesema zao la Soya uzalishaji wake umekuwa ukikuwa mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2015 hadi 2016 uzalishaji ulikuwa tani 6000.
Lakini kwa mwaka 2019 uzalishaji umefikia tani 14000, na baadhi ya Mikoa inayozalisha kwa wingi hapa nchini ni Pamoja na Iringa,Njombe, Rukwa na Songea huku akibainisha kuwa soko la zao hilo kwa hapa nchini uhitaji wake ni mkubwa sana.