Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukrani Manya wa kwanza kutoka kushoto akiwatunuku wanafunzi wa Chuo cha Madini tawi la Dodoma (hawapo pichani) wakati wa mahafali ya pili ya Chuo hicho, mahafali yaliyofanyika katika ukumbi wa TAG Miyuji Jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Madini tawi la Dodoma bwana Elvanus Kapira akitoa hotuba wakati wa mahafali ya pili ya Chuo cha Madini tawi la Dodoma, mahafali yaliyofanyika katika ukumbi wa TAG Miyuji Jijini Dodoma.
.Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es saalam UDSM Profesa William Anangisye akitoa hotuba wakati wa mahafali ya pili ya Chuo cha Madini tawi la Dodoma, maafali yaliyofanyika katika ukumbi wa TAG Miyuji Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukrani Manya wa tano kutoka kushoto waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa mahafali ya pili ya chuo cha madini tawi la Dodoma, mara baada ya kumalizika kwa mahafali katika chuo hicho mahafali yaliyofanyika katika ukumbi wa TAG Miyuji Jijini Dodoma. Baadhi ya wahitimu wa mahafali ya pili ya Chuo cha Madini tawi la Dodoma wakiwa katika picha mbili tofauti wakati wa mahafali yao yaliyofanyika katika ukumbi wa TAG Miyuji Jijini Dodoma.
**************************************
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Wahitimu wa kozi mbalimbali kutoka Chuo cha Madini wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kwa manufaa ikiwamo kulinda rasilimali za taifa na kuepuka kutumia vibaya rasilimali za taifa kwa kutumia vibaya elimu yao.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Madini tawi la Dodoma bwana Elnanus Kipara wakati wa mahafali ya pili ya kuwaaga wanafunzi 907 katika chuo hicho ambapo amesema wanaamini wametoa elimu bora na kuwajengea uwezo wa kulinda rasilimali za taifa.
“Tumewapa elimu iliyobora tunatamani mkawe kioo katika jamii hatuamini kama mtakwenda kutumia elimu yenu kulihujumu taifa” amesema Kipara.
Amebainisha kuwa wanaamini chuo kimewapa wahitimu hao silaha iliyo bora ya kwenda Kupambana na umaskini wanauwezo wa kwenda kuajiriwa serikalini na hata sekta binafsi au kujiajiri wenyewe.
“Kwa elimu hii tuliyowapa tunaamini sasa wameiva kikamilifu hapa unapowaona wanauwezo wa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe na wakapata kipato” amesema.
Aidha amewataka wahitimu hao kutoridhika na kiwango hicho cha elimu bali pindi wanapopata mda wasisite kujiendeleza na kwenda kupata digree ya kwanza katika fani walizosomea.
Mbali na hilo Kaimu Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa chuo hicho kilianzishwa rasmi mwaka 1982 na kikiwa na wanafunzi 61 kwa lengo la kutoa mafunzo ya ufundi Sanifu wa Madini hapa nchini na kimekuwa kikikuwa mwaka hadi mwaka na kufungua matawi mbalimbali ikiwamo tawi la Dodoma.
Amesema mwaka 2002 chuo kilibadilisha na kuanza kutoa elimu ya mafunzo ya fani hizo kwa miaka mitatu na mwaka 2005 kilisajiliwa rasmi na balaza la ufundi na mafunzo ya ufundi na mpaka sasa kipo chini ya ulezi wa Chuo kikuu cha Dar es saalam UDSM.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar es saalam UDSM Profesa William Anangisye amesema Wizara ilikikabidhi chuo cha madini kwa UDSM na kubainisha kuwa kwao ni furaha na nimafanikio makubwa kwa kutoa mchango katika sekta ya Madini hapa nchini.
Amesema kwa mwaka huu UDSM imeanzisha shule ya Madini ambapo chuo cha madini kitakuwa sehemu ya shule hiyo katika kuendeleza sekta ya Madini hapa nchini na kutoa mchango katika kukuza pato la taifa.
Akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake bwana Chaangaja Msuya amewashukuru wakufunzi wa chuo hicho kwa malezi mazuri kwa mda wote wakiwa masomoni na kuahidi watakwenda kuyafanyia kazi yale yote ambayo wamefundishwa kwa maendeleo ya taifa.
Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia serikali ya Tanzania na ujasili aliouchukua kipindi cha janga la Corona hali iliyopelekea wao kuhitimu mafunzo yao bila kikwazo.