Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
******************************************
Na. Abdulrahman Salim
Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa – Rukwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa Suala la ujenzi wa madarasa linakuwa agenda ya kudumu katika vikao vyote vya kisheria vya halmashauri kwakuwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kujiunga na shule imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema kuwa mbali na ujenzi huo wa madarasa mkoa una jumla ya kata 27 ambazo hazina shule za sekondari na hivyo kuwaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha kuwa kata hizo zinakuwa na shule za Sekondari hata ikibidi kuanza kwa ujenzi wa madarasa manne ili ifikapo mwaka 2022 madarasa hayo yaweze kuchukua wanafunzi 200 katika shule hizo mpya.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani humo kushiriki katika jitihada mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya shule kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule na kukumbusha kuwa ushiriki wa shughuli za maendeleo ni jukumu la kila mwananchi.
“Ndugu wajumbe hatuwezi kwenda kwa zimamoto, kila ifikapo mwishoni mwa mwaka tunaanza maagizo kama haya, hakuna likizo, hakuna nini, kamata kamata sijui nini, mkurugenzi ujenge vyumba vya madarasa kuna upungufu kama vile hatujui, tunafahamu kwamba tunayo changamoto ya vyumba vya madarasa kwa kila halmashauri, sasa ni jukumu letu sisi viongozi kuhakikisha kwamba hatuendi kwa ‘pressure’ tunajipanga tangu mwanzoni mwa mwaka mpaka mwisho,” Alisisitiza.
Halikadhalika alisema,” Naagiza Wazazi na Walezi kuhakisha Wanafunzi waliochaguliwa wanaripoti kwa asilimia 100 katika shule walizopangiwa na kwa mujibu wa ratiba ya kufungua Shule tarehe 11 Januari, 2021 na katika hili Wakuu wa Wilaya wachukue hatua kali kwa Wazazi watakaoshindwa kuhakikisha vijana wao wanaripoti katika shule walizopangiwa kwa kuwafikisha katika vyombo vya Sheria.”
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa William Mwaisumo alisema kuwa baadhi ya changamoto zinazokwamisha maendeleo ya taaluma mkoani humo ni Pamoja na baadhi ya wazazi ama walezi kutosimamia ipasavyo watoto wao baada ya kuhitimu Darasa la Saba hivyo baadhi ya watoto kutoripoti kutokana kupata mimba au baadhi yao kupelekwa kufanya kazi mashambani, majumbani au machungani.
“Tafsiri potofu ya dhana ya Elimu bila Malipo hii hupelekea baadhi ya wazazi kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya shule, na wengine kutokuwajibika kikamilifu katika usimamizi wa watoto wao hasa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo mahitaji ya shule na chakula hivyo Jamii wanatakiwa kuelewa dhana ya Elimu bila Malipo kuwa haindoi wajibu wa wazazi na wanajamii kushiriki kwenye masuala ya maendeleo ya shule na haindoi wajibu wa wazazi kwa watoto wao ikiwemo suala la kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo chakula,” Alisema.
Wakati akitoa neno la Shukurani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mh. Pancras Maliyatabu alisema kuwa kama viongozi wa kisisasa watajitahidi kuwaelekeza wazazi kuwatimizia Watoto wao mahitaji ya msingi ili waendelee kufanya vizuri katika masomo yao.
“Lakini Katika ujenzi wa upungufu wa vyoo na madarasa tutaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya kujitolea nguvu zao ili baadae serikali ije ijazie kumalizia ujenzi wa madarasa ili kutengeneza mazingira mazuri uya Watoto kusomea,” Alisema.
Wanafunzi 16,540 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mkoani Rukwa kati ya wanafunzi 17,104 waliofaulu mtihani huo wa kumaliza Elimu ya Msingi huku wanafunzi 564 wakikosa nafasi katika awamu hii ya kwanza baada ya Mkoa kuwa na upungufu wa madarasa 14 katika halmashauri ya Wialaya ya Kalambo na Manispaa ya Sumbawanga ambayo yanatakiwa kukamilika kabla ya tarehe 28.2.2021.