Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa mtaa wa Mtakuja katika kata ya Chang’ombe jijini Dodoma tarehe 18 Desemba 2020 alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu katika mtaa huo. Kushoto kwa Lukuvi ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge.
*************************************
Na Munir Shemweta, DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ametangaza eneo lenye mgogoro wa muda mrefu la Mtakuja katika kata ya Chang’ombe mkoani Dodoma kuwa la Makazi na kuanza zoezi la urasimishaji litakalookoa takriban bilioni 8.5 zilizokuwa zitumike kufanyiwa maboresho.
Eneo la Mtakuja awali lilipangwa kama eneo la ukanda wa kijani na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ajili ya kutunza mazingira na baadaye kupangwa kwa matumizi ya makuburi na kuvamiwa na hivyo kuingia katika mgogoro mkubwa na wananchi kufuatia kutangazwa kufanyiwa maboresho na halmashauri ya jiji la Dodoma.
Lukuvi alitangza uamuzi huo tarehe 18 Desemba 2020 katika mtaa wa Mtakuja jijini Dodoma alipozungumza na wananchi wa mtaaa huo akiwa katika ziara yake ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, kufuatia uamuzi wa kulitangaza eneo hilo kurasimishwa sasa eneo hilo litapimwa na kupangwa upya na hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba na kila mtu atapata haki yake.
Kwa mujibu wa Lukuvi, timu ya wizara kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Dodoma itaanza kazi ya urasimishaji wiki ijayo na kukamilika mwishoni mwa mwezi februari 2021 kwa wananchi kupatiwa hati za umiliki.
“urasimishaji utakaofanyika utafuta maendelezo ya kila mwenye eneo bila kubomoa nyumba ya mtu, tunataka kila mwanachi apate haki yake na awe na uhakika wa makazi yake ya kuishi” alisema Lukuvi
Aidha, Waziri wa Ardhi alisema kila mwananchi katika eneo la Mtakuja atalazimika kugharamia gharama za upimaji mpaka umilikishwaji na zile kodi za kisheria na kusisitiza kuwa anaamini hakuna mwananchi atakayeshindwa kulipia.
Lukuvi alibainisha kuwa, kwa wale wananchi waliopewa maeneo lakini hawakujitokeza wakati wa uhakiki zoezi la utambuzi litaendelea ili kila mmoja apate haki yake. Wananchi 867 wamehakikiwa kati ya 1049 na hivyo kufanya wananchi 182 ndiyo pekee wasiohakikiwa.
Kufuatia uamuzi wa kutangaza eneo la Mtakuja kurasimishwa sasa hati zote za wamiliki wa ardhi katika eneo hilo zimefutwa. Eneo hilo lilikuwa na jumla ya hati 65 zilizokuwa zimetolewa kwa baadhi ya wananchi wa Mtakuja.
Waziri Lukuvi alitangaza pia kufanyika uhakiki upya katika maeneo ya wananchi waliopitiwa na barabara za mzunguko katika eneo la Mtakuja ambapo awali uhakiki ulifanywa na Wakala wa Barabara TANROADS. Kwa mujibu wa Lukuvi lengo la kufanya uhakiki upya ni kubaini udanganyifu uliofanywa na baadhi ya wananchi wasio waaminifu waliokuwa na lengo la kujipatia kiasi kikubwa cha fedha ya fidia.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge alilitaka jiji la Dodoma kuhakikisha maeneo yenye maboresho yanafanyika kwa kasi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kama ilivyokuwa kwenye eneo la Mtakuja alilolielezea madhara yake yametokana na uzembe wa kutofanya maboresho mapema.
Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo alimpongeza Waziri wa Ardhi William Lukuvi kwa juhudi kubwa alizozifanya hadi kuutatua mgogoro huo ambao uhakiki wake ulikwama mara mbili mpaka alipoingilia kati.