Benki ya CRDB imeendesha Warsha ya CRDB Malkia iliyokutanisha pamoja Wanawake
Wafanyabiashara zaidi ya 250 Wilaya ya Kahama kwa ajili ya Kutambulisha bidhaa za
Malkia ambazo ni mahususi kwa mwanamke kwa ajili ya kutoa suluhu ya changamoto
zote wanazozipata wanawake katika kufikia huduma za kibenki hususani kupata
mitaji na kujiwekea akiba kwa njia rafiki.
Warsha hiyo
yenye lengo la kutoa mwanga mpya katika jitihada za kumkomboa na kumuwezesha
mwanamke wa Kitanzania kiuchumi na kijamii imefanyika leo Jumamosi Desemba
19,2020 katika Ukumbi wa Nitesh Mjini Kahama ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa
wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha.
Akifungua
Warsha ya CRDB Malkia, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha ameipongeza
Benki ya CRDB kuwa Benki ya Kizalendo iliyo mstari wa mbele kuwawezesha
wanawake wa kitanzania lakini pia kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya
tano kuwainua kiuchumi wanawake.
Macha alisema
utafiti unaonesha biashara zinazomilikiwa na wanawake ni ndogo na zenye ukuaji
hafifu akibainisha kuwa wanawake wengi wamekuwa wakikosa fursa muhimu za
kujikuza kiuchumi kwa sababu mbalimbali ikiwemo mila na desturi zenye kuwatenga
na ufahamu mdogo wa masuala ya fedha na uwekezaji.
“Tafiti
zinaonesha licha ya kuwepo wanawake wengi wanaojishughulisha kiuchumi wengi
hawatumii huduma za kibenki hasa kukopa na kuweka akiba. Zaidi ya asilimia 80%
wanatumia kukopa fedha kwenye mifumo na taasisi zisizo rasmi matokeo yake biashara hazikui kwa kasi
inayotakiwa kutokana na riba kubwa zinazotozwa na taasisi hizo zinazotoa mikopo umiza”,alisema Macha.
Alisema
taasisi za Kifedha kama Benki ya CRDB zina jukumu la kutoa elimu juu ya huduma
mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake lakini pia kubuni
bidhaa rafiki zinazoendana na mahitaji ya wanawake na zitakazosaidia kujumuisha
wanawake wengi zaidi katika mfumo wa fedha.
Mkuu huyo wa
wilaya ya Kahama aliwasihi wanawake wote wilayani Kahama kujitokeza kwa wingi
kuchangamkia fursa za uwezeshaji zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia ‘CRDB
Malkia’ na wajiunge katika umoja ulioanzishwa na Benki ya CRDB ‘Malkia
Business Club’.
“Naomba
kutoa rai kwa Benki ya CRDB kufikisha elimu juu ya huduma za CRDB Malkia kwa
wanawake wote Tanzania,mijini na vijijini. Wanawake wamekuwa wakiachwa nyuma
kidogo,niwaombe muandae warsha na fursa hizi za uwezeshaji wanawake ziwafikie
na wao pia”,aliongeza Macha.
Macha
alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanawake kuepuka kutumia fedha za mikopo kwa
mambo ambayo hawakupanga kuyafanya huku akiwataka watu wanaotoa mikopo kwa njia
zisizo rasmi kuacha mara moja kwani ni taasisi za kifedha pekee ndiyo
zinaruhusiwa kutoa huduma ya mikopo.
Kwa upande
wake, Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana amesema Benki ya CRDB imeanzisha akaunti maalumu ya
wanawake inayoitwa Malkia ambapo zaidi ya wanawake 25,000 nchi nzima wanatumia
akaunti hiyo na kujiwekea malengo sambamba na mikopo ya uwezeshaji wanawake
wafanyabiashara (WAFI) ambapo tayari benki imeshatoa mikopo yenye thamani ya
zaidi ya shilingi Bilioni 500.
Alisema Benki
ya CRDB imekuwa ikiwapeleka wanawake wajasiriamali katika mafunzo na maonesho
ndani na nje ya nchi ili kupata uzoefu na kujifunza kwa vitendo.
Pia Wagana aliwasisitiza wanawake hao kuendelea
kujiwekea akiba kwenye akaunti zao ili waweze kuibuka washindi wa kampeni ya
JIPE 5 inayomuwezesha mmliki wa akaunti ya CRDB Kujishindia pesa pindi akiweka pesa katika akaunti yake
kupitia tawi, wakala au kwa njia ya simu.
Akitoa mada
kuhusu CRDB Malkia, Meneja Uwezeshaji Wanawake Benki ya CRDB, Rachel Senni
amesema wanawake ni wafanyabiashara wazuri hivyo kupitia Akaunti ya Malkia
inayofunguliwa kwa shilingi 5000/= tu na haina makato kwa mwezi na unawekewa
faida kila mwaka kulingana na pesa ulizoweka kwenye akaunti.
“Hii ni
akaunti ya malengo binafsi na familia yako ambapo unaweza kuweka kuanzia
shilingi 1,700/= na akaunti yako ikifikisha shilingi 100,000/= unaanza kuwekewa
faida. Inasaidia kufikia malengo binafsi au ya familia lakini pia Bidhaa za Malkia
zinakuwezesha kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, kurasimisha biashara”,aliongeza
Senni.
Alifafanua
kuwa lengo la CRDB Malkia ni kuleta uwiano kiuchumi kati ya wanawake na wanaume
ili kufikia usawa wa kiuchumi na kwamba Benki ya CRDB imeleta mpango wa Malkia kwa sababu inamjali mwanamke
na inaonesha kwa vitendo kuwa kuwa mwanamke ni wa thamani.
Pia alisema
Benki ya CRDB itazindua mfumo utakaoendelea kuwaweka wanawake pamoja ‘Networking’
ili kuwa na mwendelezo wa ufuatiliaji na mafanikio ya shughuli zao.
Kwa upande
wa wanawake walionufaika na mikopo ya Benki ya CRDB akiwemo Aisha Salum, Rehema
Maharage na Kakusima Alex aliwataka
wanawake wanaokopa fedha benki kutumia fedha walizokopa kwa shughuli
walizopanga kufanya ili kupata mafanikio na si vinginevyo.
“Pesa ya
mkopo siyo ya kwenda kushonea sare. Pesa ya mkopo ifanye kazi
uliyoiombea,angalia kazi unayotaka,usibadili matumizi ya biashara au kazi
uliyopanga kufanya ili ufanikiwe. Pesa unayokopa itumie kwa kazi unayoielewa
vinginevyo utakwama”,alisema Rehema Maharage ambaye amekuwa mateja wa Benki ya
CRDB tangu mwaka 2004.