Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akizindua jiwe la Utambulisho wa eneo la Msitu wa Jiji – Medeli lenye ukubwa wa hekta 9 ambapo takribani miti 4,330 imepanda katika eneo hilo, jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Davis Mwamfupe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akipanda mti katika eneo la Msitu wa Jiji – Medeli jijini Dodoma mara baada ya kuzindua eneo hilo. Kulia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Davis Mwamfupe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi kutoka Shule mbalimbali, wawakilishi Ofisi za Jiji na Wakala wa Misitu Tanzania mara baada ya kuzindua jiwe la Utambulisho wa eneo la Msitu wa Jiji – Medeli jijini Dodoma kwa kushirikiana na Kampuni ya Vodacom; WWF na Jiji la Dodoma.
*************************************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu amesema mazingira safi, salama na endelevu ni sehemu muhimu ya kuijenga Tanzania ya Viwanda.
Hayo ameyasema hii leo Jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa eneo la mradi wa upandaji miti na kuhifadhi mazingira katika eneo la medeli lenye ukubwa wa hekta 9 ambapo takribani miti 4,330 imepandwa katika eneo hilo.
Amesema, jitihada zilizofanywa na kampuni ya Vodacom na WWF ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kutekeleza azma ya agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa mwaka 2017 katika uzinduzi wa kampeni ya Kijanisha Dodoma.
“Kuna uhitaji mkubwa wa kuboresha Mazingira ya mkoa wa Dodoma kwa kuotesha miti kwa wingi; kuhakikisha inakua na kuhifadhi Mazingira yetu, hivyo nitoe rai kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii, Asasi za Kiraia, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutathmini utekelezaji wa mkakati wa kupanda na kutunza miti wa mwaka 2016 -2021” alisisitiza Mhe. Ummy.
Amesema ili kampeni ya kijanisha Dodoma ifanikiwe ni jukumu la kila mwana Dodoma na wadau kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha Mazingira ya Dodoma.
“Kwa kuwa niña dhamana ya Kusimamia masuala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira, nitoe pongezi za dhati kwa Kampuni ya Vodacom; WWF na Jiji la Dodoma kwa juhudi mlizoonesha katika kusimamia utekelezaji wa mradi huu wa upandaji miti ambao ni muhimu kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho” Mhe. Ummy alisisitiza.
Kwa upande mwingine Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe ametoa rai kwa watanzania kubadili dhana ya kupanda miti na kuwa kuamua kustawisha miti huku akitoa rai ya kuanzishwa kwa mashindano ya upandaji miti mashuleni.
Kampuni ya simu ya Vodacom kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) na Jiji la Dodoma wameuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa kutekeleza mradi wa upandaji miti katika eneo la Medeli na maeneo mengine Jijini Dodoma