*********************************
*Ni kuhusu ujenzi wa vyumba vya madarasa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini zihakikishe zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa liwe endelevu kwa sababu idadi ya wanafunzi walioandikishwa na wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza inafahamika kupitia mitihani ya majaribio.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Desemba 18, 2020) baada ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Buhongwa iliyoko kwenye halmashauri ya jiji la Mwanza. Shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu ikiwemo madarasa.
“Ni lazima Mtoto wa Kitanzania aliyefaulu aende sekondari, jukumu la halmashauri ni kuhakikisha inajenga vyumba vya kutosha vya madarasa. Ifikapo Februari 28, 2021 ujenzi wa vyumba vya madarasa uwe umekamilika na kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kuingia darasani.”
Pia, Waziri Mkuu amewataka walimu waendelee kufanyakazi kwa bidii na kwamba Serikali inatambua na kuthamini kazi nzuri wanayoifanya ambayo inawezesha kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu kila mwaka.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi hasa wa kike wahakikishe wanatimiza ndoto zao kielimu na wasikubali kurubuniwa. “Lazima mtoto wa kike alindwe ili aweze kutumiza ndoto zake na Serikali imetunga sheria kali kwa atakayewakatisha masomo.”
Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Bw. Kiomoni Kibamba alisema jiji hilo tayari wamejenga vyumba 67 na wamejipanga kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa vyumba 53 ili kufikisha vyumba vya madarasa 120 vinavyohitajika na ifikapo Januari 11, 2021 watoto waliofaulu waanze masomo.
Akizungumzia kuhusu hali ya ufaulu katika jiji hilo Mkurugenzi huyo alisema kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu halmashuri ya jiji la Mwanza imeshika nafasi ya tatu Kitaifa na shule ya Mazoezi Butimba B imekuwa shule ya kwanza kwa shule za Serikali Kitaifa. “Ufaulu ulikuwa asilimia 98.1.
Alisema katika shule ambazo zinaendelea kujengwa wamepeleka matofali 6,000 kwa kila shule pamoja na mifuko ya saruji 200 ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa. Matofali hayo wanayatengeneza katika kiwanda cha halmashauri ambacho kimeanzishwa kwa ajili ya ufyatuaji wa matofali wanayoyatumia kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya.