Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mahali panapochimbwa ili kusimika moja ya nguzo za daraja la Kigongo – Busisi wakati alipokagua ujenzi wa daraja la Kigongo -Busisi Mkoani Mwanza, Desemba 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama jiwe lililotolewa ndani ya maji wakati wa uchimbaji wa eneo itakaposimikwa moja ya nguzo za daraja la Kigongo- Busisi mkoani Mwanza Desemba 18, 2020. (pPcha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi, Desemba 18, 20209. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Daraja la muda ambalo linawezesha ujenzi mradi wa daraja la Kigongo-Busisi ambao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutembelea Desemba 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mtambo ukichimba mahali itakaposimikwa moja ya ngozo za daraja la Kigongo-0 Busisi wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea mradi huo, Desemba 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
**********************************
*Aridhishwa na kasi ya maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja la JPM lenye urefu wa kilomita 3.2 linalojengwa katika ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 699.
Daraja hilo linajengwa kwa lengo la kuunganisha barabara kuu ya Usagara-Sengerema litakapokamilika litakuwa la kwanza kwa urefu katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.
Pia, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu unaogharimu sh. bilioni 89.764 ambao hadi sasa umefikia asilimia 70 kwa ujumla wake.
Waziri Mkuu amekagua miradi hiyo ya kimkakati leo (Ijumaa, Desemba 18, 2020) akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Mradi hiyo yote inajengwa kwa kutumia fedha za ndani.
Baada ya kukagua miradi hiyo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wake na kwamba ujenzi huo ni mfululizo wa ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji nchini.
“Ujenzi wa miradi hii utarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi kwa sababu huwezi kupata maendeleo ya watu bila kujenzi vitu. Wananchi endeleeni kuiamini Sewrikali yenu.”
Waziri Mkuu amesema hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miradi hiyo ni ya kujivunia kwa sababu itakapokamilika itawawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo
yao kwa urahisi.
Kuhusu ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi, Waziri Mkuu amesema tayari mradi huo umeshaanza kunufaisha kwani Watanzania zaidi ya 370 wameajiriwa katika mradi huo.
Waziri Mkuu amesema tayari daraja hilo limepewa jina la Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili iwe kumbukumbu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha maendeleo nchini.
Ujenzi wa daraja la JPM unaojengwa na kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ulianza Februari 2020 na unatarajiwa kukamilika Februari 2024.
Ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu unatekelezwa na kampuni ya GAS Entec na Kampuni ya KANGNAM Corporation zote za Korea Kusini zikishirikiana na SUMA JKT.
Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu inayotarajiwa kukamilika Desemba 2021 itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari makubwa matatu na madogo 20.
Wakizungumzia kuhusu ujenzi wa miradi hiyo Wabunge wa Mkoa wa Mwanza walimpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kuwa miradi hiyo inakwenda kuboresha maendeleo ya mkoa wao.
Mbunge wa Misungwi, Alexanda Mnyeti amesema ujenzi wa mradi ya daraja la JPM ni wa ajabu na hakuna aliyefikiria kama utatekelezeka. “Mradi huu ni wa muujiza tunamshukuru sana Rais.”