Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf wakiwa katika kikao cha elimu cha Manispaa ya Mpanda
Wanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Nsemulwa wakifuatilia masomo darasani
Na Zillipa Joseph, Katavi
Matokeo ya mitihani ya kupima uelewa kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu katika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi yanaridhisha ambapo wanafunzi wamefaulu kwa wastani wa alama 68
Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Mpanda Boniface Kalulu amesema matokeo hayo ni ya mitihani ya kufunga muhula wa pili
Akizungumzia changamoto ya ufundishaji wa madarasa hayo kufuatia shule kufungwa kwa miezi mitatu mwaka huu kutokana na janga la ugonjwa wa korona Kalulu amesema walimu walipata kazi ya kuanza upya kwani watoto walio wengi hasa wa madarsa ya awali na darasa la kwanza walikuwa wamesahau hata kuandika
Hata hivyo amesema kuwa kutokana na ubongo wa watoto kuwa mwepesi watoto hawakukawia kurudisha kumbukumbu na masomo yaliendelea kama kawaida
“Unajua mtoto hana mambo mengi kama mtu mzima yeye akishika jambo ameshika” alisema
Aidha ametoa pongezi kwa walimu kwa kutia bidii katia kazi yao hali iliyopelekea matokeo mazuri
‘Cha kushanganza mwaka uliopita wanafunzi wa madarasa haya walifaulu kwa wastani wa asilimia 55 lakini pamoja na kucheza kipindi ambacho tulifunga kwa ajili ya korona wamefaulu zaidi’ alieleza
Kwa upande wake mwalimu Paskali Katona anayefundisha darasa la kwanza na la pili katika shuke ya Msingi Kashato iliyopo katika Manispaa ya Mpanda amesema uelewa wa wanafunzi uko vizuri hali iliyopelekea kupata matokeo mazuri
‘Katika madarasa yangu wanafunzi wengi wamefaulu vizuri ni wachache sana ndio maksi haziridhishi lakini hao ni wale kushika nafasi ya mwisho kila mara’ alisema mwl Katona
Baadhi ya wazazi waliofika katika shule ya msingi katavi kuchukua ripoti za watoto wao wameonyesha kuridhishwa na matokeo
Amefanya vizuri, mwaka jana alikuwa wa 21 kati ya watoto 54 lakini mwaka huu mwanangu amekuwa wa 14 kati ya watoto 52’ alisema Marsha Abdala mzazi wa Shakila Ali mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Katavi
Akieleza jitihada alizofanya kama mzazi kumsaidia mtoto kitaaluma Bi Marsha alikiri kutomsaidia mwanawe katika masomo
Kiukweli nisiongope nafasi ya kumsaidia sina sanasana niwashukuru walimu wao ndio wamefanya kazi yote’ alisema
Wanafunzi wa shule za msingi wanamaliza muhula wa pili wa masomo na kufunga shule hii leo na kuanza likizo ya takriban wiki tatu ambapo shule zitafunguliwa tarehe 11 Januari 2021