Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya mkoa huo, Dk. Binilith Mahenge akiongoza kikao cha Bodi ya Barabara ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe walipata taarifa za maendeleo ya ujenzi wa barabara mkoani humo kutoka Tanroad na Tarura jijini Dodoma.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi HappinessMgalula akisoma ajenda za kikao hicho. |
Spika wa Bunge, ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai akitoa kwenye kikao hicho |
Mratibu wa Wakala wa Barabara vijijini (TARURA) Mkoa wa
Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe akitoa taarifa kwenye kikao hicho kuhusu mipango ya utekelezaji ya miradi ya
barabara za Tarura kufikia hadi Novemba,
2020.
Mhandisi Mwandamizi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi
Jacob Mukasa akielezea katika kikao hicho , kuhusu manufaa na namna mfuko unavyopanga vipaumbele vya kutoa fedha.
Mhandisi wa Barabara wa Tanroads, Clement Ngirwa akielezea
katika kikao hicho, kuhusu utaratibu wa kupandisha hadhi barabara na majukumu ya
Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara katika Hadhi Stashiki.
Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde akichangia hoja akitaka
uwepo utaratibu wa barabara za jamii nazo kutengea fedha kwa ajili ya
matengenezo.
Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dk. Ashatu Kijaji akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Mbunge wa Chemba, Mohamed Monni, akichangia hoja wakati wa
kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makota akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wakiwa katika kikao hicho
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa
wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda akitoa
taarifa kwenye kikao hicho kuhusu mipango ya utekelezaji ya miradi ya barabara za Tanroads hadi Novemba, 2020.
Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amewaagiza Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma kupeleka taarifa ofisini kwake wakiainisha madaraja yote yaliyoharibiwa na mvua yaliyodumu kwa mda mfupi sambamba na wakandarasi waliotekeleza miradi hiyo.
Dkt Mahenge ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati wa kikao cha bodi ya mfuko wa barabara Mkoa wa Dodoma ambapo amesema kumekuwa na tabia ya wakandarasi kujenga madaraja chini ya kiwango na kusababisha madaraja hayo kusombwa na maji kwa mda mfupi.
“Nataka nipate taarifa za Wakuu wa Wilaya zote maeneo gani madaraja yamevunjika na wakandarasi waliojenga miradi hiyo pia na wasanifu wa miradi hiyo haiwezekani tutumie fedha nyingi halafu mda mfupi madaraja hayo yasombwe na maji” amesema Dkt Mahenge.
Sambamba na hilo amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa huo kujenga utaratibu wa kutembelea mara kwa mara miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuepuka ujenzi wa chini ya kiwango na miradi hewa kwenye maeneo yao.
Aidha ameziagiza taasisi za TANROADS, TARURA, TANESCO, RUWASA na Jiji la Dodoma kuandaa mipango mahususi ya namna bora ya kutekeleza miradi yao ya kutoa huduma za kijamii kwa wananchi ili kusiwepo na malalamiko ya mara kwa mara.
“Nataka muandae muongozo ambao unabainisha ni kwa namna gani wananchi watapata huduma kikamilifu katika maeneo yote, na TANROADS, TARURA na Jiji mhakikishe maeneo yote yanayohitaji taa yanawekewa haraka” amesema.
Amezitaka taasisi hizo kushirikiana katika kutoa huduma kwa wananchi na sio kila taasisi kufanya kazi kivyake na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma kwa kukosa mawasiliano kwa taasisi hizo.
Ameitaka TANROADS kuwasiliana na viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote kubaini maeneo ya barabara yanayohitaji marekebisho na kuanza kutatua mara moja bila kusubiri wananchi waanze kulalamika.
Pia ameiagiza TANROADS kuanza kuyafanyia kazi maeneo ya miji inayokuwa kwa kasi kama Kibaigwa, Mbande, Bahi na Chalinze nyama kuyaboresha maeneo hayo kupunguza magari makubwa kupaki barabarani na kusababisha ajali za mara kwa mara.
Kwa upande wake kaimu meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda, amesema kwa mwaka huu wa fedha wametengewa kiasi cha Bilioni 18,647,821, huku wakitarajia kujenga kilomita 1723.91 za barabara na madaraja makubwa na madogo 332.
Pia amebainisha kuwa wamepanga kuanza na maeneo korofi huku akibainisha changamoto kubwa ya barabara kuharibika mapema ni mifugo kupita katika barabara hizo, uvamizi katika hifadhi ya barabara na kutupa taka katika mitaro ya maji na kusababisha mitaro hiyo kuziba.
Nae mratibu wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe akibainisha kuwa wamepanga kujenga mtandao wa barabara wa kilomita 6996.25, na wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 135.56 kwa mwaka wa fedha 2021- 2022, na malengo yao ni kuboresha barabara zote kuhakikisha zinapitika.