**************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amemuelekeza mkandarasi kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza kuhakikisha Ujenzi wa Barabara ya Vingunguti kwenda Barakuda kwa kiwango Cha lami yenye urefu wa Km 2.8 inafanyika usiku na Mchana na kukamilika kwa wakati huku akieleza kuwa hataki visingizio vyovyote vya kuchelewa kwa mradi.
RC Kunenge amesema licha ya Barabara hiyo kutegemewa na wananchi pia ni muhimu kwa shughuli za usafirishaji wa Mifugo na Nyama kutoka kwenye machinjio ya kisasa Vingunguti hivyo amewaelekeza TARURA kuhakikisha wanasimamia ipasavyo Ujenzi huo.
Aidha RC Kunenge amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kusikia kilio Cha muda mrefu cha wakazi wa eneo hilo na kuamua kuwatatulia changamoto hiyo.
Pamoja na hayo RC Kunenge amewapongeza TARURA na Mkandarasi wa kampuni ya Nyanza kwa mwanzo mzuri walioonyesha huku akiwashukuru wananchi kwa ushirikiano mzuri wanaompatia mkandarasi.
Kwa upande wake Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Geoffrey Mkinga amesema Ujenzi wa Barabara ulianza November 16 na inatakiwa kukamilika na kuanza kutumika ifikapo Machi 16 mwakani na Hadi Sasa Ujenzi umefikia 30% na muda wa mkataba umefikia 25%.
Aidha Mhandisi Mkinga amesema Ujenzi wa Barabara hiyo unaenda sambamba na ujenzi wa mitaro ya Maji pamoja na kuweka taa kwakuwa Barabara hiyo inatumika masaa 24.