Mwalimu Agness Mtweve wa darasa la Jifunze Shule ya Msingi Shaurimoyo akifundisha wanafunzi wake katika moja ya darasa la Jifunze shuleni hapo. |
Mwalimu Castory Mhagama wa darasa la Jifunze Shule ya Msingi Shaurimoyo akimwelekeza jambo mwanafunzi wake katika moja ya darasa la Jifunze shuleni hapo. |
Mwalimu Agness Mtweve wa darasa la Jifunze Shule ya Msingi Shaurimoyo akifundisha wanafunzi wake huku wakiimba na kujifunza kutamka katika moja ya darasa la Jifunze shuleni hapo. |
Na Joachim Mushi, Ludewa
MAJARIBIO ya mradi maalum wa darasa la Jifunze unaotekelezwa katika Shule tano za Msingi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ukiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wa kuanzia darasa la tatu hadi la sita yameonekana kuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi tangu kuanzishwa kwa mradi huo unaoratibiwa na Taasisi ya Uwezo Tanzania.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni katika shule zinazotekeleza mradi huo, wilayani hapa idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa na changamoto ya kutomudu kusoma na kuandika imepungua kwenye shule hizo, jambo ambalo limewavutia walimu kutaka mradi huo wa majaribio uwe endelevu na utekelezwe katika shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Shaurimoyo, Senebius Mtega anasema mradi wa darasa la Jifunze ulianza kutekelezwa katika shule hiyo Mwezi Agosti 2020 ukiwa na wanafunzi 78 wasiojua kusoma na kuandika katika hatua mbalimbali. Anasema wapo wanafunzi ambao walikuwa wanashindwa kusoma herufi, wengine pia kushindwa kusoma maneno na pia wapo ambao walishindwa kusoma aya; ambapo wote waligawanywa kulingana na changamoto zao za ujifunzaji.
Mwalimu Mtega anabainisha kuwa darasa la Jifunze ambalo hutekelezwa na walimu maalum waliopata mafunzo limekuwa msaada mkubwa shuleni hapo, kwani shule hiyo awali kikata ilikuwa ikiongoza kwa idadikubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika, lakini tangu uletwe mradi huo yameanza kuonekana mabadiliko chanya.
Anafafanua kuwa, darasa hilo huendeshwa kwa siku 10 mara tatu kabla ya kufanyika kwa tathmini ya kina ya kimaendeleo ya ujifunzaji wa wanafunzi hao. Anasema ndani ya siku 20 za mafunzo hayo shuleni hapo wanafunzi 48 walikwisha fuzu vizuri kusoma na kuandikwa na kuenguliwa kwenye darasa hilo. Hadi zinamalizika siku 30 za mafunzo ni wanafunzi nane tu ndio walisalia ambao bado wanaendelea kunolewa na walimu wa darasa hilo.
Afisa Elimu Kata ya Lugarawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Saidi Nyingo akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani) hivi karibuni wilayani Ludewa. |
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Shaurimoyo, Senebius Mtega akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani) hivi karibuni wilayani Ludewa. |
Afisa Elimu Kata ya Lugarawa miongoni mwa kata zinazokabiliwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Saidi Nyingo anasema katika Kata hiyo, mradi wa darasa la Jifunze uliendeshwa kwenye shule mbili. Anazitaja Shule zilizoingia katika mradi ni Shule ya Msingi Matika na Shule ya Msingi Shaurimoyo.
Anasema katika shule zote mbili jumla ya wanafunzi waliobainika hawajui kusoma na kuandika walikuwa 153 ambao waliingizwa moja kwa moja katika darasa la Jifunze kwa ajili ya kupatiwa mafunzo kulingana na changamoto zao kimadaraja. Kati ya wanafunzi hao wapo ambao walikuwa na tatizo katika kusoma maneno, wengine kusoma silabi na aya; ambapo walipagwa ili kurahisisha ujifunzaji wa darasa hilo.
Bw. Nyingo anaeleza kuwa hadi zinakamilika siku 30 za utekelezaji wa mradi wa darasa la Jifunze ni wanafunzi 22 tu ndio walisalia hawajui kusoma na kuandika katika shule hizo mbili. Taarifa zinaeleza bado na hawa wanaendelea kusaidiwa na walimu wa darasa la Jifunze ili kuhakikisha na wao wanaondokana na changamoto hiyo.
“…Kimsingi mradi wa darasa la Jifunze umeleta tija sana, kwenye maeneo yetu na umekuwa na mabadiliko makubwa. Mradi umeleta hamasa kwa watoto wanaojifunza, pia kwa walimu pamoja na wazazi. Wapo wazazi wamekuwa wakitufuata na kutueleza wazi mafanikio ya watoto wao baada ya kuhudhuria darasa la Jifunze. Wanasema kwa jinsi walivyokuwa wakiwafahamu watoto wao na changamoto ya kutojua kusoma hawakuamini kama wangebadilika kwa muda mfupi kama ilivyotokea,” anasema kiongozi huyo wa elimu ngazi ya Kata.
Anaongeza kuwa huwenda mbinu na namna ya ufundishaji umechangia kuleta mabadiliko zaidi, kwani darasa hili limeonekana kupendwa zaidi na wanafunzi. Ndani ya darasa hili mwalimu ni rafiki wa karibu wa mwanafunzi wanafunzi wanajifunza kwa vitendo, ambapo anaanza kutenda mwalimu na baadaye mwanafunzi mmoja mmoja. Wanajifunza kwa nyimbo huku akicheza jambo ambalo umvutia zaidi mwanafunzi, wanajifunza kwa ushirikiano huku wakiwa pamoja licha ya kwamba wanatoka madarasa tofauti tofauti.
Mwalimu Andrea Mhagama wa darasa la Jifunze katika Shule ya Msingi Matika akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni. |
Hata hivyo, anasema ni darasa lenye mvuto zaidi kwani huwavutia wanafunzi wengine. Darasa la Jifunze linapokuwa likifanywa katika shule hizi utawaona wanafunzi wengine wameacha shughuli zao nje na kwenda kuchungulia madirishani wenzao wanavyojifunza. Wanashuhudia wanavyojifunza kwa nyimbo na vitendo vya kuvutia. Wanafunziwanapojibu na kupata maswali wamekuwa wakituzwa kwa mtindo mbalimbali, na mwalimu hatumii fimbo katika darasa hilo kiasi cha kuonekana rafiki wa karibu wa mwanafunzi.
Chefasi Mdesa ni Mwalimu Mkuu Msaidizi Shule ya Msingi Maholong’wa, anasema Shule hiyo ni miongoni mwa Shule za Msingi zilizofanikiwa kupitiwa na mradi wa darasa la Jifunze, ambapo shughuli rasmi za darasa hilo zilianza mwezi Septemba 2020 huku wakiwa na wanafunzi 83 ambao walibainika hawajui kusoma wala kuandika. Wanafunzi wa Jifunze walianza rasmi masomo shuleni hapo Septemba 14, 2020 huku wakifundishwa kwa siku kumi kabla ya kufanyiwa tathmini ya ujifunzaji kulingana na madaraja yao.
Mwalimu huyo anafafanua kuwa hadi zinamalizika siku 30 za mradi kati ya wanafunzi 83 walioingia katika darasa hilo ni wanafunzi 26 tu ndio walisalia wakiwa na changamoto ya kutojua kusoma na kuandika ambao bado wanaendelea kusaidiwa na walimu wao ili waweze kufuzu kama wenzao. Anasema hatua hiyo ni mafanikio makubwa ukilinganisha na tatizo hilo awali kabla ya ujio wa mradi wa Jifunze.
“…Ukiniuliza maoni yangu juu ya mradi huu nitakujibu ni mzuri umeleta mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi (Siku 30 tu) na nashauri uendelee na pia uenezwe katika shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa. Na mbinu hizi hizi zinazotumika kuwafundisha watoto hawa sasa zitumike kwa wanafunzi wetu wa madarasa ya awali, darasa la kwanza pamoja na darasa la pili kwani utawasaidia sana watoto wetu,” alisema Bw. Mdesa akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi.
Anasema katika utekelezaji wa mradi huo unaosimamiwa na Uwezo zipo changamoto kidogo zimejitokeza, ikiwemo baadhi ya wazazi kutotoa ushirikiano mzuri kwa shule hasa kuwanunulia vifaa wanafunzi, kama vile madaftari maalumu ya kujifunza kuandika, kalamu na hata kutowabadilishia wanafunzi sare pale zinapo chakaa kutokana na wanafunzi hao muda mwingi kuutumia wakiwa wamekaa chini. Pamoja na hayo anasema changamoto hizo haziwezi kuzidi manufaa ya faida kwenye mradi.
Mmoja wa wanafunzi wa darasa la Jifunze akipongezwa kwa kufishwa kofia ya kifalme baada ya kujibu swali vizuri darasani. |
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la Jifunze Kata ya Lugarawa wakifuraia jambo na mwalimu wao katika picha. |