Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akimjulia hali mmoja wa majeruhi Shakila Kassim ambao wamelazwa katika hospitali ya Mtakatifu Gasper iliyopo Halmashauri ya Itigi mkoani Singida. Baadhi ya viongozi wa dini waliofika katika ibada ya kuaga miili ya marehemu 15 waliopata ajali iliyohusisha gari ndogo aina ya Hiace iliyokua ikitoka Mkoani Mwanza kuelekea Itigi kwenye harusi kugongana uso kwa uso na lori eneo la Mkiwa Wilaya ya Ikunga Mkoani Singida.Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akiwafariji wafiwa mkoani Singida kabla ya kusafirisha miili ya marehemu 15 waliopata ajali iliyohusisha gari ndogo aina ya Hiace iliyokua ikitoka Mkoani Mwanza kuelekea Itigi kwenye harusi kugongana uso kwa uso na lori eneo la Mkiwa Wilaya ya Ikunga Mkoani Singida.
…………………………………………………….
Na Majid Abdulkarim, Singida
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameshiriki katika ibada ya kuaga miili ya marehemu 15 waliopata ajali iliyohusisha gari ndogo aina ya Hiace iliyokua ikitoka Mkoani Mwanza kuelekea Itigi kwenye harusi kugongana uso kwa uso na lori eneo la Mkiwa Wilaya ya Ikunga Mkoani Singida.
Akiwafariji wafiwa amesema kuwa Serikali iko pamoja na ndugu wa marehemu kuhakikisha miili hiyo inasafirishwa kuelekea Mkoani Mwanza na Mbeya kwa ajili ya kuhifadhiwa katika nyumba zao za milele.
Dkt. Gwajima kabla ya kuaga miili hiyo ametembelea majeruhi wawili ambao ni aliyekuwa bwana harusi Herry Mkamwa na ndugu yake Shakila Kassim ambao wamelazwa katika hospitali ya Mtakatifu Gasper iliyopo Halmashauri ya Itigi mkoani Singida.
“Majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu, afya zao zinaimarika na baadae watasafirishwa kupelekwa Bugando kwa matibabu zaidi”, ameeleza Dkt. Gwajima.
Vile vile Dkt. Gwajima ameupongeza uongozi wa mkoa, viongozi wa dini na wataalamu wa afya kwa jitihada walizofanya katika kuokoa majeruhi na kuwasitiri waliotangulia mbele za haki.