******************************************
Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Mhe. Mizengo Peter Pinda ameushukuru Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kutimiza ndoto yake ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kilimo kwenye Ukanda wa ziwa Nyasa.
Shukrani hizo amezitoa Jijini Dodoma wakati akizungumza na Mwandishi wa Habari wa SUAMEDIA Calvin Gwabara juu ya Umuhimu na malengo ya uwepo wa Chuo Kikuu. ha Kilimo kwenye Ukanda huo ambao una fursa nyingi za Uzalishaji wa mazao ya kilimo na Mifugo.
Mhe. Pinda alisema kuwa alipokuwa bado serikalini alikuwa na wazo la ukanda huo kuwa na Chuo kikuu cha Kilimo lakini walikwama na baada ya hapo aliona atoe shukrani kwa Mungu na wananchi wa ukanda ule kutokana na nafasi waliyompatia Serikalini kwani ametoka pale na amekulia pale lakini pia wao ndio waliomfanya afike nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu wa Tanzania.
Alisema aliona ajenge shule ya Msingi ya kisasa wazo ambalo liliungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo na kufanikiwa kupata fedha za kujenga Madarasa 26,Nyumba za walimu 28, Chumba cha TEHAMA, Maktaba na miundombinu mingine yote ya kisasa.
Mhe. Pinda aliongeza kuwa wakati anataka kukabidhi shule hiyo yakaja mawazo mbalimbali kutoka kwa wadau na kutaka eneo hilo liwe chuo kikuu kutokana na miundombinu mizuri iliyokuwepo na akakubali na hivyo wazo likaja kuwa kuwa chuo cha kuzalisha wataalamu wa afya lakini halikufanikiwa maana Wizara ya afya walisema kwa wakati ule walikuwa wanafufua na kukarabati vyuo vyao.
” Mimi kwa upande mmoja nilifarijika sana na wazo la kuwa Chuo Kikuu na kwamba ile ndoto yangu lakini baadae tukazungumza na Viongozi wa SUA wakaja kuona na kukubali kuanzisha chuo cha kilimo nikafarijika zaidi kuona sasa tunapata Chuo Kikuu kwenye kata niliyotoka mie” Alisema Mhe. Pinda.
Aliongeza ” SUA walijiambia wanaanza na Wanafunzi 400 na unaweza kuona watoto 400 kwenye kata pale matokeo yake ni nini wanapoingia kutafuta mahitaji yao wataboresha biashara na uchumi wa watu lakini kubwa zaidi ni watoto kutoka ukanda ule watahamasika na kujiunga sana na elimu ya juu kwenye Chuo hiki na kisaidia kusukuma kilimo, Mifugo, Uvuvi katika jitihada za kuondoa umasikini kwa watu wetu”
Waziri Mkuu huyo Mstaafu amewashukuru viongozi wa SUA kwa kukubali kuanzisha Chuo Kikuu hicho cha Kilimo lakini pia Uongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambao ndio waliobeba agenda nzima na kutoa baraka za Chuo Kikuu hicho kuanzishwa.
” Nitumie fursa hii kumshukuru Rais wangu kwa sababu alipokuwa kwenye ziara alipofika kibaoni na kuona majengo yake alinipigia simu kutaka kujua ni majengo ya nini na nikakualeza ndoto yangu na aliposikia sasa SUA wanaanzisha Chuo Kikuu alifurahi na kusema waweke masuala ya Kilimo, ufugaji wa nyuki pamoja na uzalishaji wa vyakula” Alieleza Mhe. Pinda.
Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Kampasi hiyo ya Mizengo Pinda imeanza kuchukua wanafunzi mwaka huu wa 2020 katika kozi tatu ambazo ni Astashahada ya Uongozaji watalii na Uwindaji, Stashahada ya Kilimo na Shahada ya Nyuki na mazao