Na Dotto Mwaibale, Singida.
KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa Frederick Ndahani amewataka vijana waliohitimu kidato cha nne kuwa wazalendo wa nchi yetu.
Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wanafunzi wa sekondari mkoani hapa ambao ni wanachama wa Klabu ya Fema.
“Tunapaswa kuwa wazalendo wa nchi yetu na uzalendo unatafusiri nyingi kwanza unapaswa kuipenda nchi yetu kuifahamu kuithamini na kuitunza” alisema Ndahani.
Alisema wakiwa kama vijana waliohitimu kidato cha nne na wale ambao wanaendelea na masomo ni lazima kwanza wawe wazalendo.
Alisema sisi tupo katika Taifa la Tanzania hivyo hatuna Taifa lingine zaidi ya Tanzania hivyo tunapaswa kulitunza.
Alisema vijana wengi wamepoteza uzalendo kwani wanaweza kuona miundombinu imeharibika na inaibiwa wakawa hawana mpango wa kuirekebisha na kusema potelea mbali jambo ambalo si nzuri.
Ndahani aliwaambia vijana hao kuwa uzalendo unatakiwa kuuanza wakiwa na umri mdogo na kuwa hawawezi kuwa wazalendo pasipo kulielewa Taifa lao kuanzia historia yake, misingi na jinsi lilivyopatikana.
“Niwaombe ninyi wahitimu na nyie mnaoendelea na masomo ni lazima mfahamu historia ya taifa letu kwani leo hii mpo hapa mna enjoy kwa kucheza mziki na kubadilishana mawazo kuna watu waliteseka kuliangaikia taifa letu akiwepo Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere na wenzake.
Alisema ni muhimu kwa vijana hao kusoma masomo ya uraia ili waweze kulielewa taifa lao kwani wakilielewa wataweza kulitetea ndani na nje ya Tanzania.
Alisema kulielewa somo la uraia ndilo litakalowafanya waujue uzalendo wa nchi yetu ulivyo na kuwa Rais wetu Dkt.John Magufuli ni moja ya kiongozi ambao ni wazalendo wa taifa letu ambaye anaonesha uzalendo mkubwa kwa kusimamia rasilimali zetu yakiwemo madini hivyo ni lazima wawe wazalendo wa nchi.
Ndahani aliwataka vijana hao kutii sheria na kuacha kujiingiza katika vitendo vya uvutaji wa bangi, ukahaba, ushoga, wezi na vingine hivyo aliwaomba
kutumia muda wao kwa kucheza mpira kuliko kufanya vitendo hivyo ambavyo vitaweza kuharibu tabia zao.
Aidha Ndahani aliwaambia vijana hao kuwa wanao uwezo wa kuanzisha na kubuni shughuli ndogo ndogo za kiuchumi ambazo zinaweza kuwaingizia kipato kama ufugaji wa kuku, sungura na kilimo badala ya kukaa vijiweni wamepoteza muda.
Ndahani aliwataka vijana hao kulinda afya zao ili watimize ndoto zao kwani kama viongozi hawa waliopo wasinge linda afya zao tusingekuwa nao leo hii.
Mwenyekiti wa Fema Mkoa wa Singida, Donald Adam alitoa rai kwa vijana hao waliohitimu kidato cha nne kuwa wakawe wabunifu na watafiti katika kujishughulisha na kazi halali zitakazowapatia kipato kwa lengo la kusaidia jamii na Taifa la Tanzania.
Alisema vijana hao watumie dhana ya 4H (4Hhead, health, haert, na hands) wakiwa mashuleni pamoja na akili, utashi kujifunza zaidi kwa vitendo wajali afya zaidi na wasijihusishe na ngono zembe na wawe na moyo wa kujitolea na kusaidia wahitaji ikiwa ni agenda ya sema tenda na kwa mikono yao wajikite kufanya kazi kwa bidii ili kujisaidia wenyewe na jamii kwa ujumla .
Adam aliwataka wahitimu hao Wakawe mabalozi katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unaisha katika jamii wanayotoka na kuwa wao kama Fema wanayo kazi ya kujenga Taifa imara na la kizalendo.