Diwani wa Kata ya Kabwe kwa tiketi ya CHADEMA Mh. Asante Lubinsha akila kiapo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Wilaya ya Nkasi pamoja na wananchi na uongozi wa Halmashauri na Mkoa.
Diwani wa Viti Maalum CCM Mh. Jenifrida Mhagama akila Kiapo chake mbele ya Jaji Mfawidhi wa Wilaya ya Nkasi pamoja na wananchi na uongozi wa Halmashauri na Mkoa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mh. Pancras Maliyatabu akitoa ahadi ya kutekeleza maelekezo yote ya Uongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na kutimiza ahadi walizotoa kwa wananchi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
*********************************
Baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa wametakiwa kukahikisha kila Kijiji na Kata katika maeneo yao kunakuwa na shule za Msingi na Sekondari ili kuwaepusha Watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu na hivyo kukutana na vikwazo vingi hali inayowapelekea wengine kushindwa kukamilisha masomo yao na kuishia kuolewa ama kupata mimba.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo terehe 15.12.2020 alipokuwa akitoa nasaha zake baada ya madiwani wa Baraza hilo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kumaliza kula viapo vyao mbele ya wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Wakati akielezea hali ya miundombuni ya elimu katika halmshauri hiyo Mh. Wangabo alisema kuwa Halmashauri hiyo yenye Vijiji 90 inatakiwa kuwa na Shule 90 za Msingi lakini kinyume chake ni vijiji 74 pekee ndio vyenye shule hizo huku vijiji 16 vikiwa havina shule za Msingi.
Na kuongeza kuwa Kata 21 pekee kati ya Kata 28 za Halmshauri hiyo ndio zenye Shule ya Sekondari na hivyo kuziacha Kata 7 zikiwa hazina Shule ya Sekondari jambo linalowasababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu huku wakiwa hatarini kukumbana na wasiopenda maendeleo ya elimu kwa Watoto wakiwasuburi kuwatia mimba na hivyo kuwataka Madiwani kushirikiana na wananchi kutatua changamoto hiyo.
Aidha aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Nkasi kwa kuweza kuwa na madarasa ya kutosheleza wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2021 na kuwasisitiza kuendelea kutengeneza madawati na viti vya kutosha kwaajili ya wanafunzi hao.
“Nendeni mkasimamie kata zenu ziwe na shule za Sekondari, hizi kata saba ziwe na shule zake za Sekondari, Sasa hivi tunahangaika Mh. DC amesema hapa, kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliofaulu wanakwenda Sekondari, ninyi hapa nawapongeza hakuna tatizo hilo kwa upande wa wanafunzi waliochaguli kwenda kidato cha kwanza wakakosa nafasi, mko vizuri, ila mkaangalie suala la madawati na viti na kukamilisha vyumba ambavyo mshaanza kuvijenga,” Alisema.
“Na pale ambapo kuna Sekondari hakuna bweni, kajengeni bweni ili Watoto wa mbali na wenyewe wapate mahali pa kuishi salama, huko kwenye vijumba vya kupanga si salama, mtoto unampeleka akiwa vizuri anakurudishia mimba kisa ni mazingira haya ya kutolea elimu sio mazuri, chukueni hili mkalifanyie kazi,” Alisisitiza.
Akielezea Mkakati wa Wilaya kuhusu kuhakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kuingia kidato cha kwanza anakaa kwenye dawati Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mh. Said Mtanda alisema kuwa watendaji wa halmashauri hiyo watafanya ziara katika shule zote za sekondari ili kuhakikisha wanafunzi hao wanakaa kwenye madawati.
“Kwahiyo watendaji wa Halmashauri tumekubaliana utekelezaji tarehe 28.1.2021. atakayeshindwa kwenda na kasi ya utekelezaji wa mipango hiyo tumekubaliana kama ni mratibu wa elimu ya Kata na kata yake haina madawati kitakachofuata ni tutafute mbadala wake naye tumtafutie shule akafundishe kwasababu hatuna njia nyingine kwa sasa, hatuwezi kuendelea na mwendo wa kubembelezana kwenye maendeleo,” Alisema.