******************************************
Na Mwandishi wetu, Simiyu
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amezitaka halmashauri zote nchini kujitathmini kwa kuweka mikakati ya muda mfupi ya kufanya mapinduzi ya utoaji huduma za afya kwa wananchi ili kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana wakati wote.
Dkt. Dugange amebainisha kauli hiyo leo wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Simiyu.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa kufanyike marejeo ya bajeti “budget reallocation” kwa kuzingatia maslahi mapana ya mahitaji ya vifaa tiba ili kuviwezesha vituo vya afya vipya vilivyojengwa na serikali ya awamu ya tano kutoa huduma walau ya wagonjwa wa nje (OPD) kwa kuanzia.
Aidha Dkt. Dugange ameelekeza halmashauri kuhakikisha mifumo ya ukusanyaji mapato inasimikwa na kutumika kikamilifu kwenye vituo vya afya vyote nchini ili kudhibiti upotevu wa fedha za makusanyo ya papo kwa papo.
“Usimikwaji wa mifumo katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini itasaidia kutatua changamoto ya ulaji wa “pesa mbichi” na badala yake fedha hiyo itafikishwa sehemu sahihi na kuelekezwa katika maendeleo ya taifa”, amesisitiza Dkt. Dugange.
Lakini pia Dkt. Dugange ameongeza kuwa mifumo hiyo itapunguza utegemezi kutoka serikali kuu na itaimarisha uwezo wa kifedha wa vituo vya afya na hatimaye kufanya mapinduzi ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kuwa imara na wakika.
Vile vile ametoa wito kwa timu za afya mkoa na halmashauri kufanya uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (ICHF) ili kuwawezesha upatikanaji wa matibabu kwa grama nafuu na uhakika wa huduma za afya wakati wote.
Awali kabla ya kikao hicho Dkt. Dugange amepata wasaa wa kukagua hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu ambapo amezungumza na wafanyakazi pamoja na wananchi wa maeneo hayo.
“Nia ya dhati ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha mifumo ya utoaji huduma za afya unaboreshwa ili watanzania kujivunia matunda yatokanayo na kodi zao”, ameeleza Dkt. Dugange.