Mratibu wa Upimaji wa Afya bure kwa Wakazi wa wilaya ya Meru kwenye viwanja Leganga kutoka kampuni ya Phide Phidesia Mwakitalima wakiongea na wanahabari hawapo pichani wakati wa hitimisho la zoezi hilo picha Ahmed Mahmoud Meru.
**********************************
Na Ahmed Mahmoud Arumeru
Wananchi wa Wilayani Meru Mkoani Arusha wengi wao wakiwa kutoka familia zisizo na uwezo wa kifedha wamepatiwa huduma ya matibabu ya bure ya magonjwa mbalimbali kwa siku mbili mwishoni mwa wiki.
Aidha wananchi hao wamepata huduma hiyo kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali za serikali ikionyesha idadi kubwa wakigundulika kusumbuliwa na magonjwa ya macho pamoja na shinikizo la damu hali inayotajwa kusababishwa na mfumo wa maisha wanayoishi.
Zoezi hilo limefanyika kwa siku mbili ikiwa ni siku ya ufugaji katika kiwanja cha Leganga likiwa na lengo la kuwafikia Wana Arumeru zaidi ya mia mbili wenye uhitaji wa kupata upimaji wa Afya zao hususani wenye magonjwa na wanaoshindwa kupata vipimo kutokana na kushindwa kumudu gharama za upimaji.
Matibabu hayo ambayo yameratibiwa na kampuni ya Phide kwa kushirikiana na hospital ya Mkoa ya Mount Meru,ambapo Mkurugenzi wa kampuni hiyo Phidesia Mwakitalima amesema kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza mara nyingi hayapewi kipaumbele kuwapima wananchi na hivyo wao wameonyesha njia ili kuokoa wananchi walio wengi.
Alisema kuwa kutokana na zoezi hilo wamebaini uhitaji wa wananchi wengi wanaohitaji upimaji wa Afya zao kwenye eneo la magonjwa yasioambukiza hivyo kutoa rai kwa serikali angalau mara moja kushirikiana na wadau wa maendeleo kufanya zoezi kama hilo mara kwa mara
Kwa upande wake mtaalamu wa afya kutoka hospitali ya Mkoa ya Mount Meru Juma Muna amesema kuwa uhitaji wa wananchi kupimwa magonjwa ambayo si ya kuambukizwa ni mkubwa na kwamba kitendo hicho ni kuonyesha kujali afya za wananchi hasa wenye hali duni.
“Vipimo hivi vya macho,presha,shinikizo la damu ,kisukari, na magonjwa ya mfumo wa hewa ni miongoni mwa magonjwa yanayosumbua Sana jamii yetu kwa kuwa wengine hushindwa kupima kutokana na umbali wa hospitali ama fedha,kwa hiyo fursa hii itumiwe na wadau wengine kufanya zoezi kama hili ikiwemo na uchangiaji damu”Alisema Juma
Vile vile baadhi ya wananchi waliopatiwa huduma hiyo wamesema upimaji huo imekuja wakati muafaka kwa kuwa wengi wao hawana uwezo wa kifedha kugharamia matibabu hayo katika maeneo yao wanayoishi ikiwemo pia umbali mrefu kufikia maeneo ya matibabu .
Zoezi hilo ni la nne toka kuanzishwa kwa utaratibu huo wa upimaji na kampuni hiyo ambapo watu takribani mia NNE wameshanufaika na zoezi hilo na watalifanya kwa mkoa mzima wa Arusha.