*************************************
NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
MBUNGE Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameeleza, kukerwa kwake na migogoro ya ardhi isiyokwisha baina ya vijiji na vijiji ,ikiwemo ile inayohusisha mipaka na ya wakulima na wafugaji ndani ya Chalinze.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Kata ya Kimange kushukuru na kupokea kero na maoni ya wananchi Kijiji cha Pongwekiona na Kimange, Ridhiwani alieleza migogoro hiyo inavyokwamisha juhudi za kuleta maendeleo jimboni hapo.
Akizungumza kujibu hoja iliyowasilishwa na wananchi, Mbunge aliwaagiza viongozi wa Serikali za vijiji hivyo kwamba ni lazima wasimamie sheria walizojiwekea ili kuondoa migongano isiyokwisha ikiwemo ile ya Wakulima na Wafugaji.
Ridhiwani ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria, alitumia nafasi hiyo kuwashauri wananchi na hasa Serikali za vijiji hivyo juu ya umuhimu wa kufuata sheria ili kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na pia wanapotaka kujadili migogoro na vijiji vyengine.
Pamoja na kuwashauri huko kisheria, Mbunge alitumia nafasi hiyo ya ziara kuwaomba wananchi waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika juhudi zake za kuwakomboa wananchi wanyonge wa Tanzania katika ukandamizi unaofanywa na wachache wenye tamaa hasa katika Elimu, Afya, Ardhi, na kusaidia kuwakomboa wananchi katika Umaskini.
“Raisi wetu Magufuli anawashukuru sana kwa kura nyingi na amewaahidi kuwatumikia wananchi wake.Kura mlizompa ni kielelezo cha imani kubwa tuliyonayo wana Chalinze kwake na serikali yake.Mheshimiwa Rais ametuahidi mambo makubwa sana na kwa heshima hii ametuahidi hatotuacha.
Aidha, katika ziara yake hiyo kero za migogoro ya baina ya wananchi jamii ya wafugaji na wakulima ziliibuka na Mbunge ameagiza kuendelea kusimamia sheria ikiwemo sheria za Vijiji na zile za Serikali kuu ili kuleta usawa baina ya pande zote mbili.
Mbali ya kero hiyo Wananchi wa Kijiji cha Pongwekiona walimuomba Mbunge wao huyo kusimamia maboresho ya barabara inayotoka Kimange-Pongwekiona ili iweze kupitika wakati wote bila shida.
” Tumekuwa tukipata vikwazo pindi wapatapo dharura ya mgonjwa ama mama mjamzito ili kumuwaisha sehemu za huduma kama Kituo cha afya ama Hospitali ya Wilaya Chalinze,”Alisema Saumu Hamiss mkazi wa Pongwekiona.
Nae Mwanawetu Salum alisema barabara hiyo imekua kero kubwa ikiwemo kushindwa kusafirisha bidhaa zao hoja ambayo iliungwa mkono na karibu wananchi wote katika mkutano huo.
Mbunge anaendelea na ziara katika Kata mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa kukutana na wananchi kuwashukuru kwa kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi CCM na kumpatia ushindi wa kishindo Mgombea wake Dkt. Magufuli na pia kujipanga katika kutekeleza Majukumu mara baada ya kuapishwa Baraza la Madiwani.