Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akimtua mama ndoo ya maji mara baada ya kukagua mradi wa maji wa Leto wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro.
*********************************
Na Evaristy Masuha.
Mradi mkubwa wa maji wa ziwa Chala, utakaogharimu zaidi ya Sh Bilioni 34 unatarajiwa kuanza Januari 2021 na kurudisha matumaini mapya kwa wakazi wa Rombo ambao wameteseka kusaka huduma ya maji kwa miaka mingi
Hayo yamebainishwa leo Disemba 14, 2020 na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (MB) wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Kisale-Msaranga Wilayani Rombo, ambapo amesema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero ya maji.
Amesema usanifu wa mradi huo tayari umekamilika na kwamba mapema Januari 2021, serikali itatoa Sh Bilioni 2 ili kuanza hatua za awali za ujenzi wa mradi huo.
“Mradi wa Maji ziwa chala usanifu wake umekamilika, tutarajie mapema Januari 2021 Serikali italeta shilingi bilioni 2, ili kuanza hatua za awali za ujenzi wa mradi huu, na lengo ni kuona wananchi wa Rombo, wanapata huduma ya maji kwa asilimia 100.” Amesema Naibu Waziri.
Naibu waziri wa Maji yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro, ambapo mbali na kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao, amekagua vyanzo mbalimbali vya maji na kuangalia hali ya upatikanaji wa Maji katika mkoa huo.