*******************************
Dec 15
NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA
WAZIRI wa maji ,Jumaa Aweso ameiagiza mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Dar -es -salaam (DAWASA) ,kuongeza nguvu ili kukamilisha mradi wa maji Mkuranga-Vikindu awamu ya kwanza kabla ya mwezi February 2021 huku akiipongeza kwa dhamira ya kuondoa kero ya maji iliyodumu miaka mingi katika wilaya hiyo.
Akitoa maelekezo hayo akiwa Mkuranga na Kibiti ,Aweso aliitaka DAWASA pamoja na RUWASA kutupia macho na kuongeza nguvu za ziada katika wilaya ya Mkuranga,Kibiti na Ikwiriri ili kuziondolea kero ya maji safi na kuhakikisha inabaki kuwa historia.
“Mkuranga wanapata maji ,serikali imedhamiria kuleta maji,DAWASA baada ya kuwakabidhi neema inaonekana ,watu wa Mkuranga wanataka maji na sio maneno “,wananchi wamevumilia sana ,mkandarasi abanwe kuongeza nguvu ili kuanza kutekeleza awamu ya pili ya mradi.”,;
” Wataalamu wetu walituchelewesha sana ,walitupotosha vyanzo vya maji hakuna kumbe walikuwa wakila sahani moja na watu wa maboza,wauze maji kwa faida yao, na kukwamisha azma ya serikali ya kutatua tatizo la maji,lakini Leo hii tunaona muelekeo”alibainisha Aweso.
Aidha alieleza ,serikali ya awamu ya tano itaendelea kutia nguvu katika kuongeza fedha za kumalizia miradi ya maji ilihali kutimiza azma ya serikali ya kuwa na maji bombani .
Aweso pia alielekeza RUWASA ,kusimamia kurekebisha bili za maji ,ili kupunguza malalamiko ya wananchi kubambikiwa bill kubwa ama zisizoendana na matumizi yao.
Alimtaka na afisa Mtendaji Mkuu DAWASA kuongeza mikoa ,hatua itakayowezesha kufikia maeneo mengi na kumtua ndoo mama kichwani maeneo ya pembezoni.
Pamoja na hayo,Aweso alimuagiza meneja wa RUWASA Mkoani Pwani ,Beatrice kusimamia upatikanaji wa maji eneo la Mwanambaya na kumuomba awe na mapembe kwa watendaji wa chini ambao wataonekana wanakwamisha miradi ya maji.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu (DAWASA) mhandisi Cyprian Luhemeja alipokea maelekezo na maagizo yote kutoka kwa Waziri na kusema wanaahidi kumaliza mradi wa maji Mkuranga mwezi February na endapo mkandarasi ataongezewa fedha haraka utakamilika kabla ya mwezi huo.
” Mradi huu utakapokamilika awamu ya kwanza utatoa huduma kwa wakazi 25,500 kwa gharama ya bilioni 5.5, pia tutaanza maandalizi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi awamu ya pili utakaopeleka maji mpaka kwenye tanki kubwa lakini eneo la Mwanambaya ,Kisemvule ,Vikindu ,Mwandege ,Kipara Mpakani na maeneo ya pembezoni kwa barabara kuu “alifafanua Luhemeja.
Meneja wa RUWASA Kibiti, Clement Kivegaro alieleza ,wanatekeleza mradi kwa kutumia watumishi wa ndani ,hawatumii mkandarasi kwa gharama ya sh.milioni 382.1 ,na mradi huo umefikia asimilia 75 kukamilika.
Mbunge wa jimbo la Kibiti, Twaha Mpembenue ,aliipongeza RUWASA na wizara ya maji na kusema wanahitaji milioni 849.1 kwa mwaka mpya wa fedha,ambapo zikipatikana zitasaidia miradi ya maji Mjawa,Mtunda na Mahege ili wananchi wanufaike na huduma ya maji safi.