**************************************
Na Mwandishi wetu, Kiteto
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kiteto, MkoaniManyara, Mheshimiwa Mosi Sasi amemuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya laki tano Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Kata ya Bwawani Wilayani Kiteto Steven Tadayo Tollya.
Tadayo alifikishwa Mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wakili Yahya Masakilija kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu ishirini kinyume cha k/f cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11/2007.
Tadayo aliomba rushwa hiyo kwa mwananchi mmoja kwa maelezo kwamba ni gharama ya kufungua shauri pamoja na kuwa mwananchi huyo tayari alikuwa ameshatoa elfu Kumi kabla ya madai hayo ya Rushwa ya elfu ishirini,
Hata hivyo, Tadayo ameweza kulipa laki tano na kukwepa adhabu ya kutumikia kifungo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Makungu ametoa wito kwa wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata kujiepusha na tabia za kudai rushwa kwa kuwa wananchi sasa wana uelewa wa kutosha kuhusu rushwa na mahali pa kutoa taarifa.
“Kwa wenye kushupaza shingo wafahamu kuwa wataendelea kuharibikiwa kwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria,” amesema Makungu.