*************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wastahiki Meya, Makatibu Tawala na Wakuu wa Idara kuhakikisha wanasimamia kikamilifu majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi yote yenye kutatua kero za wananchi inakamilika.
RC Kunenge ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua miradi Wilaya ya Kinondoni ambapo akiwa kwenye kiwanda Cha kuchakata mbolea itokanayo na taka zinazozalishwa Jijini humo kilichopo Mabwepande RC Kunenge ameelekeza Manispaa ya Kinondoni kuwaondoa wote waliovamia na kujenga kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 14.
Aidha RC Kunenge ameitaka Manispaa hiyo kuhakikisha Kiwanda hicho kinaanza kufanya kazi kabla ya Mwezi February mwakani ambapo ameelaeza kuwa uwezo wa Kiwanda utakuwa ni kuchakata tani 50 za taka na kupata tani 30 za mbolea kwa siku.
Akiwa kwenye Mradi wa Ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Kinondoni RC Kunenge ameelekeza pia Manispaa hiyo kuhakikisha shughuli za Ujenzi zinafanyika usiku na Mchana ili iweze kuanza kutoa huduma February mosi mwakani na kubainisha kuwa hospital hiyo itakuwa mkombozi kwa wananchi wa maeneo ya jirani ambapo kwa mujibu wa Manispaa ya Kinondoni Ujenzi huo utagharimu shilingi bilioni 2.5 ikiwa ni fedha za ndani.
Pamoja na hayo RC Kunenge ametembelea kituo Cha Afya cha Bunju A na kutaka kianze kutoa huduma ifikapo February mosi mwakani ambapo amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa kiasi Cha shilingi milioni 600 za Ujenzi wa kituo hicho ili wananchi wapate huduma Bora za Afya.
Katika hatua nyingine RC Kunenge amewataka wananchi kuzingatia suala la usafi wa mazingira kwa kuhakikisha wanasafisha mazingira yao kwakuwa usafi ni wajibu wa kila mmoja na kusisitiza kuwa yoyote atakaebainika kuchafua mazingira kwa namna yoyote ile ikiwemo utiririshaji wa maji machafu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria pasipokujali wadhifa au nafasi yao katika jamii.