*****************************
Na Mwandishi wetu, Kiteto
MADIWANI na Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, wamepatiwa mafunzo ya ushiriki wa kila mmoja kupambana na rushwa, yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Manyara.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza kwenye mafunzo hayo amewahimiza madiwani kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili kufanikisha ilani ya CCM ambayo ndiyo inaongoza Serikali.
Makungu amesema popote pale wakibaini miradi yenye dalili za kuhujumiwa na wakandarasi wasio waadilifu au inayoonekana kujengwa chini ya kiwango, watoe taarifa TAKUKURU kwa simu namba 113 ambayo haihitaji kulipiwa.
Amesema TAKUKURU ndicho chombo chenye mamlaka kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2017 kuongoza vita dhidi ya rushwa Tanzania bara.
Amesema sheria ya manunuzi inazuia halmashauri kufanya manunuzi kwa waajiriwa wa halmashauri au makampuni ya madiwani au kampuni za wabia wa madiwani.
“Hapa watendaji kama Mkurugenzi wa halmashauri, mhasibu, mhandisi, mkuu wa kitengo cha manunuzi huingizwa kwenye uhalifu huo ambao mara nyingi manunuzi na zabuni hutolewa kwa makampuni ya madiwani au jamaa zao ambao huwa asilimia 10,” amesema Makungu.
Amesema matokeo yake miradi husika hujengwa chini ya kiwango kwa kuwa fedha nyingine haziendi kwenye miradi hiyo zinaingia mifukoni mwa madiwani na hakuna wa kumfunga paka kengele.
“Ndiyo maana utashangaa miradi iliyo chini ya kiwango baadhi yenu hufumbia macho hadi iibuliwe kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais mwenyewe, wakati madiwani wapo na miradi hiyo ipo maeneo yenu,” amesema Makungu.
Hata hivyo, amesema pia tatizo lipo kwenye mazingira ya baadhi ya madiwani waliopita kwa njia ya rushwa, ikitokea watendaji wa halmashauri wamekataa kuwa sehemu ya uovu utasikia kikao cha madiwani kimewaazimia kwa kudai hawapati ushirikiano kwani kuna baadhi ya maeneo wakurugenzi na wakuu wa idara wamefanyiwa hivyo na ukiuliza madiwani wanadai Mkurugenzi au Mkuu wa idara hana ushirikiano.
Amesema katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto lililopita baadhi ya madiwani walishirikiana na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na baadhi ya watendaji wa serikali ngazi ya vijiji na kata walikuwa chanzo cha migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima, kijiji na kijiji au mtu na mtu.
“Ukiwa wewe ni Diwani unahamasisha wananchi wakalime msitu wa hifadhi ya jamii kama vile Suledo, wakalime WMA au Emboley Murtangos fahamu kuwa unatumia mamlaka yako vibaya na unaweza kushtakiwa chini ya sheria kifungu cha 31/PCCA 2007,” amesema Makungu.
Amesema baadhi ya madiwani kwenye baraza lililopita wanaotoka kwenye kata zenye minada wanarudisha nyuma maendeleo kwa kuweka watu wao wanaowapa sehemu ya fedha za ushuru badala ya kukusanya na kufikisha halmashauri.