*************************************
✔Watoa maelekezo mahususi
Na Teresia Mhagama, Dodoma
Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt Medard Kalemani pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato wamefanya kikao kazi cha kwanza na Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na kutoa maelekezo mbalimbali ikiwemo kutoa ukomo wa ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 12 Disemba, 2020 katika Ofisi za Wizara ya Nishati, zilizopo Mtumba jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara na Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi.
Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi hizo, wanatoka, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
Waziri wa Nishati amesema kuwa, ili nchi iweze kuwa na nishati ya kutosha, ni muhimu miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo ya umeme na gesi ikakamilika kwa wakati na ameagiza mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2115 ukamilike ifikapo tarehe 14 Juni 2022.
Aidha, amesema kuwa, maandalizi ya mradi wa umeme wa Ruhudji yalishaanza hivyo alitoa agizo kuwa, manunuzi ya mradi huo utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 358, yakamilike ifikapo mwezi Juni 2021 kwani kipaumbele ni kuwa na umeme wa kutosha nchini.
Pia ameagiza kuwa, mradi wa umeme wa Rumakali utakaozalisha megawati 222, uanze kwani lengo la Serikali ni kuwa na umeme wa kutosha utakaotosheleza mahitaji.
Vilevile, kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi I Extension utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 185, ameagiza kuwa, ukamilike ndani ya miezi Sita kutoka sasa.
Akizungumzia kuhusu mradi wa usambazaji umeme vijijini, Waziri Kalemani ameagiza kuwa, vijiji 2288 ambavyo havijasambaziwa umeme, viwe vimeunganishwa na umeme ifikapo mwezi Desemba mwaka 2022 ambapo mpaka sasa Vijiji 9980 tayari vimesambaziwa nishati ya umeme.
Dkt. Kalemani pia ameagiza kuwa, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Kidahwe-Kigoma na ule wa Ipole mkoani Tabora hadi Katavi, yote ikamilike ndani ya miezi minane ili mikoa yote Tanzania Bara iwe imeunganishwa na gridi ya Taifa.
Suala la wateja takribani 16,000 ambao wameshalipia huduma ya umeme na bado hawajaunganishwa, Waziri Kalemani ameagiza kuwa, wawe wameunganishwa na huduma hiyo ndani ya miezi minne.
Aidha, ameagiza kuwa ndani ya miezi sita kuanzia sasa, Ofisi za TANESCO zinapaswa kuwepo kwenye majengo ya Shirika badala ya kupanga kwenye majengo ya watu binafsi ili kuweza kuokoa fedha za Serikali.
Vilevile kwa wateja wanaodaiwa na TANESCO, Dkt. Kalemani ameagiza kuwa, wote wakatiwe umeme, iwe Taasisi za Umma au binafsi kwani zinahitajika fedha za kujenga miradi mbalimbali ya umeme.
Waziri wa Nishati pia ameziagiza Ofisi za TANESCO katika wilaya zote kuwa na stoo ya kuhifadhi vifaa vya umeme kama vile transfoma ili kuwa na utatuzi wa haraka pale inapotokea changamoto ya vifaa vya umeme kuharibika na kukosesha wananchi huduma ya umeme.
Kuhusu Mafuta na Gesi Asilia, Waziri Kalemani amesema kuwa, TPDC wajikite katika masuala ya uchimbaji baada ya kufanya tafiti nyingi kwani gesi inahitajika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani na pia wananchi wanatarajia kuona mafuta hivyo ndani ya miezi Saba kuwe na dalili za uchimbaji wa mafuta.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta hadi vijijini ili kuwaondolea adha wananchi ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo, Dkt. Kalemani ameiagiza EWURA kutoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ndani ya miezi mitatu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato alimshukuru Waziri wa Nishati kwa maelekezo yake na kueleza kuwa yupo tayari kuyatekeleza kwa kasi, ubunifu na usahihi kwa kushirikiana na watendaji wa Wizara na Taasisi.
Kuhusu kuanzisha, kuendeleza na kumalizia miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme kwenye maeneo ya mijini na vijijini amesema kuwa atasimamia utekelezaji wa suala hilo.
Aidha, suala la umeme kukatwa kwa wateja wanaodaiwa na TANESCO, amesisitiza kuwa, agizo hilo la Waziri wa Nishati, lifanyiwe kazi kwa kuwa miradi ya umeme na Gesi ili itekelezwe, inahitaji fedha.
Kuhusu wateja takribani 16,000 waliolipia huduma ya umeme na hawajaunganishwa hadi sasa, amesisitiza kuwa, waunganishwe na huduma hiyo ndani ya miezi minne na kuongeza kuwa kuwa, wateja hao ni wale waliopita na wa sasa.
Aidha, amesema kuwa, atafuatilia suala la uwepo wa vifaa vya umeme katika ofisi za TANESCO nchini kwani uwepo wa vifaa hivyo utasaidia katika upelekaji wa huduma kwa haraka kwa wananchi.
Vilevile, amesema kuwa, umeme utaendelea kusambazwa katika visiwa mbalimbali nchini kwa gharama stahiki.
Kikao cha Waziri wa Nishati na Naibu Waziri wa Nishati pamoja na Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati ni cha kwanza kufanyika mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwaapisha kushika nyadhifa hizo tarehe 9 Disemba, 2020.
Caps
moja
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Medard Kalemani akizungumza katika kikao na Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato.
Mbili
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, akizungumza katika kikao na Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Medard Kalemani.
Tatu
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao cha Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato na Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma.
Nne
Baadhi ya Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Medard Kalemani pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato. Kikao kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma.
Tano
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (kulia), Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo (wa pili kutoka kulia), Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi (wa pili kutoka kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka wakiwa katika kikao cha Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato na Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma.