Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa Carolyne Nombo, akihutubia kwenye mahafali ya 18 ya Taasisi hiyo kwa Kampasi zake za Singida, Mwanza na Kigoma mkoani Singida juzi.
Baadhi ya wahitimu wa Cheti cha Awali cha Uhasibu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wa Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma wakisubiri kutunukiwa vyeti vyao kwenye mahafali ya 18 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika mkoani Singida juzi.
Brass Band ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ikiongoza maandamano ya wahitimu hao kabla ya kuanza kwa mahafali hayo.
Viongozi mbalimbali kuroka Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma wakiwa wamejipanga mbele ya Jukwaa kuu wakati wa kumpokea mgeni rasmi wa mahafali hayo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAHITIMU
wapatao 2485 kutoka Taasisi ya Uhasibu nchini, Kampasi za Singida, Mwanza na
Kigoma wametunukiwa vyeti vya fani mbalimbali, ikiwemo vile vya awali,
astashahada, stashahada na shahada-katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi,
Uongozi wa Rasilimali Watu na Usimamizi wa Biashara.
Katika
sherehe hizo za mahafali ya 18 zilizofanyika kwenye viwanja vya Kampasi ya
Taasisi hiyo mkoani hapa juzi, imeelezwa kwamba, kutokana na maboresho kadhaa
ya miundombiu ya kielimu idadi ya wanaodahiliwa imeendelea kupanda mwaka hadi
mwaka.
Akihutubia
mahafali hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA nchini, Profesa Carolyne Nombo
alisema mathalani, kwa mwaka 2019/20 wanachuo waliodahiliwa kwenye kozi
mbalimbali kwa kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma pekee walikuwa 2,700.
“Hili ni
ongezeko la asilimia 29.9 ukilinganisha na wanachuo 1,894 waliodahiliwa katika
mwaka wa masomo 2018/19. Ongezeko hili ni matokeo ya ubora wa elimu
inayotolewa, utaratibu mzuri wa serikali kupitia (TAMISEMI) na ongezeko la
mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada,” alisema Prof. Nombo.
Akifafanua
zaidi, alisema ubora wa elimu inayotolewa na Taasisi hiyo unatokana na mitaala
inayowajengea wanachuo wake umahiri (competency) na hivyo kumwezesha mhitimu
kuajiriwa au kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake.
Aidha,
Nombo alisema binafsi anafarijika na utaratibu mzuri wa serikali kupitia
(TAMISEMI) wa kuwapangia vyuo moja kwa moja wale wahitimu wa kidato cha nne
waliofaulu na kukidhi vigezo.
“Mathalani,
katika mwaka wa masomo 2020/21 jumla ya wanafunzi 2557 kutoka maeneo mbalimbali
nchini wamepangwa kujiunga na kozi mbalimbali za cheti cha awali,” alisema.
Imeelezwa
kati ya idadi hiyo, wanafunzi 1200 wamepangwa katika kampasi ya Singida, na
wengine 398 kampasi ya Mwanza huku idadi ya 957 ikipangwa Kigoma.
Pia Nombo
alipongeza juhudi za serikali, kipekee Rais John Magufuli, kwa maono yake
chanya kwenye sekta ya elimu, hususani kwa namna alivyotoa msukumo wa kipekee
kwenye ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada.
“Katika
kuhakikisha tunaunga mkono jitihada za serikali katika kuleta ustawi mzuri wa
elimu, kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma zimeweza kutembelea shule
mbalimbali za sekondari kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma, na kuwaeleza
fursa za masomo zilizopo TIA,” alisema.
Awali, kupitia mahafali hayo, Naibu Katibu
Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga, alisema serikali ipo
tayari kutoa kila aina ya ushirikiano ndani ya TIA na wahitimu wake, kwa
kuzingatia fani zinazotolewa zina umuhimu mkubwa kwa ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Endeleeni
kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na kubuni mbinu mpya, fani zinazotolewa TIA
ni muhimu sana katika kuendesha uchumi wa taifa letu na kuhakikisha matumizi
bora ya fedha za umma,” alisema Maganga.
Katika
hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo kwa niaba ya Wizara ya Fedha, alipongeza
mchango wa TIA katika kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo, wakulima,
wafugaji, wavuvi na vikundi vya ushirika.
“Jitihada
hizi ni za muhimu sana katika lengo la Taifa la kurasimisha shughuli za
wajasiriamali wadogo, na pia ni maagizo ya Rais Magufuli katika shabaha iliyopo
ya kuwawezesha kupatiwa huduma muhimu ikiwemo mikopo,” alisema.
Hata
hivyo, Meneja wa Kampasi ya Singida, Abbas Sanga, alisema TIA imejipanga
vizuri, na kwamba mpaka sasa inaendelea kuwa kitovu katika kuhakikisha tija ya
mafunzo yake inajikita katika mantiki ya uhalisia wa ustawi wa maisha punde tu
mwanafunzi anapohitimu.
“Lengo
letu ni kuendelea kutoa wahitimu wenye stadi stahiki za kumudu kufanya kazi
mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri, lakini shabaha ni kuendelea kuhuisha
mitaala yetu ili iendane na mahitaji ya kitaifa na kimataifa,” alisema Sanga.
TIA ina
jumla ya Kampasi 6 zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Singida,
Mtwara, Mwanza na Kigoma zikiwa na jumla ya wanachuo 18,717.