Mahafali yakiendelea. Wa tatu kulia waliosima ni Mhitimu wa Shahada ya Uongozi na Rasilimali Watu, Caroline Mduma.
|
Waratibu wa Taaluma wakiwa kwenye mahafali hayo.
Na Dotto
Mwaibale, Singida
TAASISI
mahiri na kongwe ya uhasibu nchini (TIA) ipo mbioni kuanza ujenzi wa baadhi ya majengo
yake kwenye kampasi yake iliyopo jiji la Mwanza, baada ya taratibu zote za
michoro kukamilika.
Taasisi hiyo
kwa sasa imezidi kupanua wigo wa kimafunzo sanjari na kujiimarisha katika
mifumo ya utoaji elimu kuendana na teknolojia za kisasa, lengo ni kuongeza tija
na kujenga uwezo kwa muhitimu kuwa mahiri na mbunifu.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa Carolyne Nombo, aliyasema hayo mkoani hapa juzi, wakati
akihutubia mahafali ya 18 ya Taasisi hiyo kwa Kampasi zake za Singida, Mwanza
na Kigoma.
“Katika
mwaka wa fedha 2020/2021 Taasisi imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa
ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, maabara ya kompyuta na maktaba baada ya
kufanikiwa kupata hati za viwanja vyake vilivyopo Luchelele na Nyang’homango,” alisema Prof. Nombo na kuongeza:
“Pia
taasisi imetenga kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya ujenzi wa kantini
na nyumba za watumishi katika eneo lake la Nyang’homango wilaya ya Misungwi na
michoro imekamilika.”
Alisema
kwa upande wa kampasi yake ya Kigoma TIA kwa mwaka huo huo wa fedha 2020/2021
imetenga shilingi milioni 450 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la taaluma,
baada ya kufanikiwa kununua eneo lililopo Kamara ndani ya Halmashauri ya Wilaya
ya Kigoma.
Nombo
alisema kwa upande wa kampasi ya Singida tayari wamekamilisha jengo la Maabara
ya kisasa ya Kompyuta na Maktaba zenye uwezo wa kuhudumia wanachuo 200 kwa
wakati mmoja.
Alibainisha
kwamba kwa mwaka wa fedha 2020/21 taasisi hiyo imetenga kiasi cha shilingi
milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Taaluma na uzio kwenye jengo la
chuo chake kwa kampasi ya Singida.
“Mafanikio
yote haya yanatokana na utendaji mzuri wa serikali ya Awamu ya Tano chini ya
uongozi wa Jemedari Rais John Magufuli ambaye wakati wote amekuwa akitoa
kipaumbele katika sekta ya elimu,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa TIA huku
akisisitiza:
“Azma yetu
ni kuhakikisha tunauhisha mitaala iliyopo ili iendane na mahitaji ya soko.
Lengo ni kuendelea kutoa wahitimu wenye stadi stahiki za kumudu kufanya kazi
mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri.”
Awali, Naibu
Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga, ambaye ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi wa mahafali hayo, alisema serikali ipo tayari kutoa kila
aina ya ushirikiano ndani ya TIA na wahitimu wake, kwa kuzingatia fani
zinazotolewa zina umuhimu mkubwa kwa ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Endeleeni
kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na kubuni mbinu mpya, fani zinazotolewa TIA
ni muhimu sana katika kuendesha uchumi wa taifa letu na kuhakikisha matumizi
bora ya fedha za umma,” alisema Maganga.
Katika
hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo kwa niaba ya Wizara ya Fedha, alipongeza
mchango wa TIA katika kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo, wakulima,
wafugaji, wavuvi na vikundi vya ushirika.
“Jitihada
hizi ni za muhimu sana katika lengo la Taifa la kurasimisha shughuli za
wajasiriamali wadogo, na pia ni maagizo ya Rais Magufuli katika shabaha iliyopo
ya kuwawezesha kupatiwa huduma muhimu ikiwemo mikopo,” alisema.
Katika
mahafali hiyo ya 18 kwa Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma, jumla ya wahitimu
2485 wamehitimu kozi za cheti cha awali, astashahada, stashahada na shahada
katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Uongozi wa Rasilimali Watu na
Usimamizi wa Biashara.