Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) na Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe (Mb) leo tarehe 10 Desemba, 2020 wameripoti katika ofisi za wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma na kupokekewa na Menejimenti ya Wizara hiyo ikingozwa na Katibu Mkuu Prof Riziki Shemdoe na Naibu Katibu Mkuu ndugu Ludovick Nduhiye.
Wakizungumza na Menejimenti hiyo baada ya kufika ofisini hapo wote kwa pamoja wameomba ushirikiano mkubwa kutoka kwa Watumishi wote wa wizara huku wakisisitiza weledi na kujituma kwenye kazi kwa kila mmoja ndio siri ya mafanikio.
Akizungumza katika kikao kifupi na watendaji hao, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mwambe amewataka watumishi wote wa Wizara ya Viwanda kuumpa ushirikiano na kufanya kazi kwa kutumia taaluma zao na kuhaidi kufanya kikao kingine na wafanyakazi wote ili kujua changamoto mbali mbali zinazowakabili watumishi na kuzifanyia kazi.
“Tunashukuru kwa mapokezi yenu yaliyojaa upendo, tunawaahidi ushirikiano, tutafanya vikao na taasisi zetu zote 15 zilizo chini ya wizara na kuzungumza na Wakurugenzi wakuu wa taasisi na pia wakuu wa Idara na vitengo” Alisema Mhe. Mwambe.
Aidha Mhe. Mwambe aliwataka wakuu wote wa Idara zinazosimamia taasisi hizo kuhakikisha zinaleta tija kwa Taifa letu na watanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe (Mb) amewaomba watumishi wote wa wizara hiyo kumpa ushirikiano kwa kuwa yeye ni mwenyeji katika Wizara hiyo na kuwataka watumishi wawe tayari kuendana na mabadiriko yalitokea na kuahidi kuwa atafanya kazi kwa weredi bila kumuonea mtu wala kuumpendelea mtu.
“Niwaombe tushirikiane kama Timu ili tuweze kufika tunapopataka, kwenye sekta zetu hizi yapo mambo ambayo yaliahidiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuomba kura kwa wananchi na yapo kwenye Ilani ya CCM, ni kazi yetu kwenda kuyasimamia na kuyatekeleza kama yalivyoelekezwa” Alisema Mhe. Kigahe.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewapongeza Mawaziri kwa kuteuliwa kwao na kuwakaribisha huku akihaidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa viongozi hao katika kuijenga Tanzania ya Viwanda.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) pamoja na Naibu waziri Mhe. Exaud Kigahe (Mb) baada ya kupokelewa na Katibu wa wizara Prof. Riziki Shemdoe pamoja na Naibu Katibu Ludovick Nduhiye na watumishi wa wizara.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) akisalimiana na wafanyakazi wa wizara mara baada ya kuwasili katika ofisi za wizara zilizoko Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) akisaini katika ofisi za wizara Mtumba na kufanya majadiliano na Naibu waziri pamoja na Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Idelphonce Mwambe (Mb) pamoja na Naibu waziri Mhe. Exaud Kigahe (Mb) wakipokea zawadi ya ukaribisho kutoka kwa mtumishi wa wizara Bi. Stella Nswima mara baada ya kufika katika ofisi za wizara Mtumba jijini Dodoma.