Na Estom Sanga – Iringa
Wajumbe wa kamati ya taifa ya Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF –NSC wamewahimiza Wananchi wanaonufaika na huduma zitolewazo na Serikali kupitia Mfuko huo kutobweteka na mafanikio waliyoyapata badala yake watumie fursa hiyo kuuchukia zaidi
umaskini.
Ushauri
huo umetolewa na Wajumbe wa Kamati ndogo ya Miradi na bajeti ya TASAF wakati wa
ziara ya kikazi katika wilaya za Mufindi na Iringa Vijijini mkoani Iringa
ambako wamekutana na baadhi ya Walengwa wa TASAF na kujionea namna walivyotumia
fursa ya kuorodheshwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Akizungumza
na Walengwa katika kijiji cha Ludilo wilayani Mufindi na Matembo katika halmashauri
ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndogo ya NSC
inayoshughulikia miradi na bajeti Dr. Naftal Ng’ondi amebainisha kuwa azma ya
Serikali ni kuona kuwa Walengwa wa Mfuko huo wanatumia kwa dhati fursa hiyo
kuondokana na umaskini.
Aidha
Dr. Ng’ondi amewataka Walengwa wa TASAF na wananchi wengine ambao watoto wao
wamepata fursa ya kuendelea na masomo ya Sekondari hapo mwakani kuhakikisha
kuwa watoto hao hawaipotezi fursa hiyo adhimu .
Wakiwa
katika kijiji cha Ludilo Wilayani Mufindi Wajumbe hao wametembelea Miradi ya
upandaji wa miti, matunda aina ya Miparachichi na mabwawa ya kufugia samaki
ambayo imetekelezwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa Miradi ya Ajira
ya Muda-PWP.
Wajumbe
hao pia wameshuhudia namna baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Matembo,
halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini
namna walivyoboresha makazi yao kwa kujenga nyumba na kuezeka kwa mabati baada
ya kupata ruzuku kutoka TASAF.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bwana Ladislaus Mwamanga amebainisha
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli ameagiza
kuwa mitaa,vijiji na shehia zote nchini zijumuishwe kwenye shughuli za Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini ili Wananchi watakaokidhi
vigezo waweze kunufaika na huduma za Mpango
huo maagizo ambayo amesema
yatatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Mmoja
wa Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Matembo, Iringa Vijijini (katikati) akiwa na baadhi ya Wajumbe kamati ya Uongozi
wa TASAF Taifa na Wataalamu wakiwa mbele
ya nyumba aliyoijenga kutokana na ruzuku anayopata kutoka serikalini kupitia
TASAF.
Baadhi
ya Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa TASAF taifa wakiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya wanafunzi wanaotoka kwenye
kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini katika kijiji cha Matembo halmashauri ya wilaya ya Iiringa
Vijijini.
Picha
ya juu na chini baadhi ya Wajumbe ya Kamati ya Uongozi wa TASAF taifa wakikagua Shamba la miti na matunda
aina ya Miparachichi ambayo imepandwa na Walengwa wa TASAF kupitia utaratibu wa
Ajira ya Muda katika kijiji cha Ludilo
wilayani Mufindi mkoani Iringa.