Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Songea na Namtumbo(Sonamcu)Juma Mwanga akielezea mafanikio ya chama hicho katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 ambapo chama hicho kupitia wakulima wake walizalisha zaidi ya tani 3,086 ya zao la Tumbaku na zaidi ya shilingi bilioni 9 zilipatikana.
****************************************
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
WAKULIMA wa Tumbaku mkoani Ruvuma ambao ni wanachama wa chama kikuu cha Ushirika cha wilaya ya Songea na Namtumbo(Sonamcu) wamejipatia zaidi ya shilingi bilioni 9 kutokana na mauzo ya tani 3,086 ya zao la tumbaku katika kipindi cha miaka 4 kutoka 2017 hadi 2020.
Mbali na wakulima,halmashauri ya Manispaa ya Songea,Halmashauri ya wilaya ya Songea na Namtumbo nazo zimepata kiasi cha shilingi milioni 250 kama malipo ya ushuru kutokana na mauzo ya Tumbaku.
Meneja Mkuu wa chama kikuu cha Ushirika Sonamcu Juma Mwanga amesema hayo jana ofisini kwake, ambapo alieleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kupatikana katika muda wa miaka mitano ya utawala wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuri.
Alisema,kuanza upya uzalishaji wa zao la Tumbaku mkoani Ruvuma kumetokana na juhudi za Chama kikuu cha Ushirika(Sonamcu) kupata mnunuzi wa uhakika kampuni ya Premium Active Tanzania Limited, ambayo imeingia mkataba wa miaka saba na chama hicho kununua tumbaku inayolimwa katika mkoa huo kuanzia mwaka 2017 hadi 2023.
Alisema, mbali na ununuzi wa zao la Tumbaku pia chama hicho kimesimamia na kuratibu masoko ya mazao ya ufuta,soya na mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao gharani.
Aidha alisema, katika kipindi hicho Sonamcu imefanikisha kuimarisha mfumo huo kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia 2019 na 2020 sambamba na kuwezesha kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao hayo pamoja na wakulima kupata fedha za uhakika ambapo Sonamcu kwa kushirikiana na serikali ya mkoa na wizara ya kilimo imesimami vema mfumo wa ununuzi wa mazao kupitia stakabadhi gharani.
Kwa mujibu wa Mwanga,Sonamcu imepewa dhamana na serikali ya kusimamia mfumo wa masoko wa stakabadhi gharani katika mkoa wa Ruvuma, ambapo imefanikisha kuhamasisha wakulima kulima mazao mengine ya biashara ikiwemo soya,ufuta na mbaazi.
Alieleza kwamba,kilimo cha mazao hayo ni mkakati mwingine unaolenga kuwaongezea kipato wakulima badala ya kutegemea zao moja la Tumbaku ambalo licha ya kuwa na soko la uhakika, lakini Sonamcu na serikali ya mkoa ikaone ni vema wakulima walime mazao mengine.
Mwanga alisema, kimsingi stakabadhi gharani ni mkombozi mkubwa wa mkulima kwa sababu umerahisisha sana suala la soko na bei nzuri ya mazao yao tofauti ambapo sasa mkulima ana uhakika wa kupata fedha na hivyo kujikwamua na umaskini tofauti na siku za nyuma.
Katika misimu miwili ya kilimo 2019/2020 wakulima walipata zaidi ya shilingi bilioni 32 kutokana na mauzo ya zao la mbaazi,soya na ufuta na halmashauri za mkoa huo zilipata zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kama ushuru jambo ambalo kabla ya mfumo huo, halmashauri hazikuweza kupata mapato makubwa.
Mwanga alitolea mfano halmshauri ya wilaya ya Namtumbo katika msimu wa kilimo 2018 kupitia zao la ufuta fedha za ushuru ilipata shilingi milioni 70, lakini baada ya mfumo huo kuanza kazi mwaka 2019 Halmashauri hiyo ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 358.
“kwa hiyo hapa unaona kabla ya mfumo ni jinsi gani watendaji wasio waaminifu wameiletea halmashauri yao hasara kiasi gani,lakini kwa mfumo wa stakabadhi gharani na ukusanyaji fedha kwa kutumia mashine za Efds tumeondoa mianya yote ya upotevu wa mapato na sasa halmashauri zina uwezo wa kuboresha baadhi ya huduma za kijamii”alisema Mwanga.
Alisema,mfumo huu umeleta tija kubwa katika mkoa wa Ruvuma, kwani licha ya kuwapatia wakulima fedha nyingi, pia zaidi ya vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) 65 vimefufuka.
Pia alisema, hii ni mara ya kwanza katika muda wa miaka kumi Chama kikuu cha Ushirika Sonamcu kupata zaidi ya milioni 500 kutokana na ushuru wa mauzo ya mazao kama tumbaku,ufuta,soya na mbaazi fedha ambazo zimekwenda kuimarisha chama hicho ikilinganisha na misimu iliyopita fedha ambazo sehemu ya fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha vifungashio kinachojengwa katika halmashauri ya wilaya ya Namtumbo”alisema Mwanga.
Mwanga, amezipongeza halmashauri za mkoa huo kwa usimamizi mzuri wa fedha zinazopatikana na kuhaidi kuwa Sonamcu itaendelea kusimamia vema mfumo wa masoko wa stakabadhi gharani katika mkoa wa Ruvuma.