Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 23 kwa wakulima watano wa Mvomelo ikiwa ni malipo ya fidia toka Shirika la Bima la Taifa (NIC) kufuatia mashamba yao uharibiwa na mvua msimu uliopita. Kulia aliyeshikana mkono ni mkulima Dorika Mlacha akiwa na wenzake Morogoro leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakulima wa Mvomelo walionufaika na Bima ya Mazao (waliosimama) leo alipowakabidhi hundi ya shilingi milioni 23 mjini Morogoro iliyotolewa na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( katikati) akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 23 kwa wakulima watano wenye Bima za Mazao kati 32 waliofidiwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kutokana na mashamba yao kuharibiwa na mvua nyingi msimu uliopita wa kilimo .Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Dkt. Elirehema Doriye na Kulia ni Mkurugenzi wa Wakala wa Mbegu (ASA) Dkt. Sophia Kashenge.
Shirika la Bima la Taifa limewalipa wakulima watano wa Mvomero jumla ya shilingi milioni 23 ikiwa ni fidia ya mazao yao kuharibiwa na majanga ikiwemo mafuriko yaliyoharibu mashamba yao ya mpunga na mahindi msimu uliopita wa kilimo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ndiye aliyekabidhi hundi ya shilingi milioni 23 kwa wakulima watano toka wilaya ya Mvomelo halfa iliyofanyika leo (11.12.2020) mjini Morogoro.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Kusaya aliwapongeza wakulima hao waliojiunga na bima ya mazao hali inayowasaidia kujikinga na majanga ikiwemo mafuriko, ukame na wadudu waharibifu wa mazao shambani.
Kusaya alibainisha kuwa siku hii inaoesha mafanikio kwa wakulima watano kati ya 32 wa Mvomero walipwa fidia ya shilingi milioni 23 kufuatia mashamba yao mahindi na mpunga kuathirika na mafuriko na visumbufu vya mimea
“ Nimejulishwa kuwa msimu uliopita wakulima 32 kutoka wilaya tofauti hapa nchini ambao walikatia bima shughuli zao za kilimo kupitia Shirika la Bima la Taifa ,mashamba yao yaliathiriwa na majanga ,hivyo leo tunawakabidhi fedha ikiwa ni fidia kwa mujibu wa sheria na mikataba na shirika letu la bima” alisema Kusaya.
Kufuatia hatua hiyo Kusaya alitoa wito kwa wakulima nchini kukata bima ya mazao yao ili iwakinge na kuwapa uhakika na usalama wa shughuli zao za kilimo.
Katibu Mkuu Kusaya aliongeza kusema wizara yake itaendelea kuhamasisha wakulima wengi wajiunge na bima ya mazao na kulitaka shirika la Bima la Taifa kwenda mkoani Katavi hususan wilaya ya Mlele ambapo wakulima wa tumbaku wa ushirika wa Ukonongo walipata hasara mwaka jana kwa mazao yao kuharibiwa na mvua hivyo wanahitaji kujiunga na Bima za mazao.
“Nataka Mkurugenzi Mtendaji na timu yako nendeni mkatoe elimu kwa wakulima wa tumbaku wa chama cha ushirika Ukonongo wilaya ya Mlele ambao wamepata hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni moja kwa tumbaku yao kuharibiwa na mvua msimu uliopita. Niliwatembelea Octoba wakasema wapo tayari kujiunga na Bima ya Mazao” alielekeza Katibu Mkuu Kusaya.
Ili kufikia malengo ya seriklai ya awamu ya tano kuongeza mabilionea kupitia kilimo Kusaya alisema ni budi wakulima kufanya kilimo biashara ambacho kinga yake ya uhakika ni kuwa na bima ya mazao .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Dkt. Elirehema Doriye alisema tangu kuanzishwa kwa huduma ya bima ya mazao jumla ya wakulima 562 wamepewa kinga ambapo wengi waliokumbwa na athari wamekuwa wakilipwa fidia ya majanga.
“Zaidi ya wakulima 562 wameweza kujiungakatika huduma ya Bima ya Mazao ikijumisha wakulima wa pamba, mpunga, mahindi pamoja na pareto” alieleza Dkt. Doriye.
Dkt. Doriye alisema jumla ya wakulima wengine 27 kati ya 32 waliokubwa na atahri mbalimbali nchini watalipwa Shilingi milioni 23 ikiwa ni sehemu ya fidia kwenye hasara iliyojitokea katika msimu wa kilimo uliopita.
Mkurugenzi huyo wa NIC alitaja mafanikio mengine ya taasisi hiyo pamoja na kutoa elimu ya bima ya mazao na faida zake kwa wakulima 10,716 wa mikoa ya Simiyu, Morogoro, Njombe na Iringa
Shirika la Bima la Taifa limefanikiwa pia kuanza kutoa bima ya kwa mazao ya kimkakati ikiwemo chai, tumbaku, mkonge, michikchi, cocoa, alizeti na miwa.
Dkt. Doriye alitoa pongezi kwa serikali kwa kuridhia na kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika bidhaa huduma ya bima ya mazao kwa mwaka 2020/21 hali inayowafanya wakulima wawe na uhakika na faida pale wanapojiunga.
“Faida za bima ya mazao ya lima salama ni pamoja na kumlinda mkulima dhidi ya mjanga ya ukame mkali, mvua kali, mafuriko, wadudu, magonjwa na moto wakati mazao yakiwa shambani “ alisema Dkt. Doriye.
Mmoja wa wanufaika wa malipo ya fidia baada ya kujiunga na bima ya mazao mkulima Dorika Mlacha toka wilaya ya Mvomero alisema tukio la kulipwa fedha limekuwa ni historia mpya kwa Morogoro na limewatia moyo wakulima baada ya kupata hasara shambani.
Dorika ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Msaidizi wa MVIWATA wilaya ya Mvomero alimweleza Katibu Mkuu Kilimo kuwa kwenye vikao vyao wakulima wengi walikuwa wakiuliza maswali mengi kuhusu faida ya bima ya mazao na kukawa hakuna majibu lakini kwa tukio la Shirika la Bima la Taifa kulipa fidia amepata majawabu.
“Leo nimekuwa shuhuda kuwa bima ya mazao kwa wakulima hususan waadogo ina faida kubwa . Nimefurahi sana kuona Katibu Mkuu ukitukabidhi fedha zetu fidia” alishukuru Dorika
Wizara ya Kilimo ilizindua rasmi huduma ya Bima ya Mazao mwezi Agosti 2019 wakati wa Maadhimisho ya sherehe za Nanenane zilizofanyika mkoani Simiyu na kuwa sasa kuwa sasa inaendealea kutoa elimu kwa wakulima kupitia mkakati na mwongozo wa bima za mazao uliosambazwa nchini kote.
Ilielezwa pia kuwa lengo la hatua za kuanzishwa kwa bima ya mazao ni kuweka mazingira wezeshi ya kutekeleza Programu ya Kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la taifa.