***************************************
(Na Lilian Shembilu- MAELEZO)
Virusi vya UKIMWI (VVU) ni aina ya virusi vinavyosababisha Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI). UKIMWI ni hatua ya mwisho ya maambukizi ya VVU ambayo hufanyika wakati uwingi wa seli za CD4 umepungua sana na baada ya hapo mtu anaanza kupata magonjwa nyemelezi.
VVU hushambulia aina za seli nyeupe za damu zinazoitwa CD4 ambazo hupigana na maambukizi. Seli hizi huitwa pia T seli, seli msaidizi, au CD4 lymphocytes.
Maambukizi ya VVU humaanisha kwamba virusi vya ukimwi vinakuwa ndani ya mwili wa mtu. Virusi hivi vikiwa ndani ya mwili wa mtu kuna baadhi ya watu watabakia na afya nzuri pamoja na kwamba wana maambukizi kwa muda mrefu, lakini wengine wanaanza kuugua mapema zaidi.
Ili mtu afahamu kuwa ana maambukizi ya VVU ni lazima aende kupima kwenye kituo cha afya au hospitali, huwezi kufahamu kama una maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kujihisi tu hata kama umejamiiana bila kinga (kondomu) na mtu unayehisi ana VVU. Mtu yeyote ambaye angependa kufahamu namna ya kuzuia VVU au mwenye hofu kuwa ana maambukizi ya VVU amwone mtaalamu wa afya au atembelee kituo cha UKIMWI ili kupata taarifa kuhusu uzuiaji wa VVU na /au ushauri kuhusu mahali anapoweza kupata huduma za kupima VVU, ushauri nasaha, uangalizi au usaidizi.
Ugonjwa wa UKIMWI hauna tiba ila zipo dawa za kufubaza virusi vinavyosababisha UKIMWI na pindi mtu mwenye maambukizi ya VVU anapoanza kupata magonjwa nyemelezi kama homa za mara kwa mara anapoumwa homa ya kuhara, anapoumwa kichwa, tumbo, anapovimba matezi, anapopata magonjwa ya kinywani, kifua kikuu, magonjwa ya ngozi (mkanda wa jeshi) na mengine mengi anaweza kupata matibabu ya magonjwa hayo.
Tanzania imeimarisha huduma za tiba ikiwemo kusisitiza matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs). Msisitizo huu umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka vifo vya watu 85,000 mwaka 2001 hadi kufikia vifo 21,529 mwaka 2019.
Mtu anaweza kupata maambukizi ya VVU kwa njia mbalimbali ikiwemo kujamiina bila kinga (kondomu ya kike au ya kiume) na mtu aliyeambukizwa VVU, na hapa ndipo vijana wengi wanapopata maambukizi ya VVU, pamoja na kuwa na wapenzi wengi, lakini pia kuna njia ya vitu vyenye ncha kali kama sindano, viwembe na njia hii inasababisha vijana wengi wanaotumia dawa za kulevya wanaojidunga sindano kuambukizana VVU kwa urahisi sana. Lakini pia mtoto anaweza kupata maambukizi kutoka kwa mama pale anapojifungua kama tahadhari haijachukuliwa na pia wakati wa kunyonyesha.
Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) wanasema bado UKIMWI ni tishio na kutokana na takwimu walizonazo katika kila watu 100, watu 4 wana maambukizi ya VVU/UKIMWI, ambapo miongoni mwa watu hao wenye maambukizi ni vijana. Takwimu za maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini Tanzania zinawataja vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 kuwa wanaongoza katika kupata maambukizi mapya ya VVU kila mwaka kwa asilimia zaidi ya 40. Asilimia 80 ya maambukizi ya kundi la vijana ni wasichana ambao huwa na wapenzi wengi na kujiweka katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Katika siku ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 1, Desemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema “Nataka nitoe tahadhari ya watu wazima wanaojihusisha na mapenzi na wasichana wadogo. Niwakumbushe kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika”.
Aidha, aliwaasa vijana kutojihusisha na mapenzi katika umri mdogo ili waweze kutimiza ndoto na malengo yao ya baadaye katika maisha yao. Aliwasihi kutodanganyika na vishawishi kutoka kwa wanaume wenye umri mkubwa wanaowalaghai na vizawadi vidogo vidogo na pesa pia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Leticia Mourice anaiomba Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini na vyombo vya habari viendelee kutoa elimu ya makuzi, kubadili tabia na hofu ya Mungu kwa vijana, wazazi na walezi ili kuepusha na matendo hatarishi.
“Hatua kali zichukuliwe dhidi ya ukandamizaji na udhalilishaji wa aina yoyote ya haki kwa watoto na vijana. Pia, viongozi wa dini, kwa kuzingatia misingi ya imani zetu, tushikamane kuelimishana na kuongoza jamii ya waumini kupiga vita unyanyapaa dhidi ya VVU” alisema Leticia Mourice siku ya maadhimisho ya UKIMWI duniani.
Ni vyema wazazi au walezi wengine wajadiliane na watoto na vijana wao kuhusu mahusiano, ngono na hatari ya kuweza kupata maambukizo ya VVU. Wasichana na kinamama wa umri mdogo ndio hasa wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizo ya VVU. Wasichana na wavulani wanapaswa waelewe kuhusu umuhimu wa usawa na kuheshimiana katika mahusiano.
Aidha, wazazi, waalimu, viongozi wa makundi rika na watu wengine wanaoheshimika wawaandalie vijana mazingira salama na kuwafundisha stadi mbalimbali zitakazowasaidia katika kujenga tabia na kufanya maamuzi salama kwa afya zao. Watoto na vijana wana nafasi muhimu katika kufikia na kutekeleza maamuzi kuhusu uzuiaji wa VVU, utoaji wa huduma na msaada unaowahusu wao wenyewe, familia na jamii zao.
Familia zilizoathirika na VVU huenda zikahitaji msaada wa kipato na wa huduma za kijamii kwa ajili ya kuziwezesha kuhudumia wagonjwa na watoto katika familia zao, hivyo ni vyema Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini zikajitahidi kutoa misaada kwa familia hizo husika.
Suala la kuzingatia ni kutowanyanyapaa wagonjwa wa UKIMWI, awe ni mtoto, kijana au mtu mzima yeyote mwenye VVU asinyanyapaliwe au kubaguliwa. Wazazi, waalimu na viongozi wana jukumu la msingi katika utoaji wa elimu ya VVU na uzuiaji wake na katika kupunguza unyanyapaa na ubaguzi.
Tangu kuingia kwa ugonjwa wa UKIMWI nchini, Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuhakikisha inafanya kila jitihada ambazo zinaweza kupunguza au kumaliza kabisa ugonjwa huu kwa kutoa elimu kupitia katika taasisi mbalimbali za kidini, mashirika ya Kiserikali na yasiyo ya Kiserikali na watu binafsi. Elimu hii imekuwa inatolewa kwa njia ya mikutano, semina, makongamano na vyombo vya habari.